Maswali magumu matano tukio la kutekwa Mo Dewji

Muktasari:

Tukio la kutekwa kwa bilionea kijana Mohammed Dewji ‘Mo Dewji’ limeacha maswali mazito ya kiusalama na kuibua shauku ya kujua kwa nini matukio ya aina hiyo hayakomi kujirudia licha ya mamlaka za usalama kuapa kuwa hayatatokea tena

Dar es Salaam. Tukio la kutekwa kwa bilionea kijana Mohamed Dewji, juzi alfajiri limeacha maswali mazito ya kiusalama na kuibua shauku ya kujua kwa nini matukio ya aina hiyo hayakomi kujirudia licha ya polisi na mamlaka za usalama kuapa kuwa hayatatokea tena.

Taarifa za kutekwa kwa tajiri huyo mwenye mguso wa pekee kwa wananchi na ushawishi mkubwa kwa jumuiya ya wafanyabiashara zilianza kuripotiwa juzi alfajiri na kusambaa kwa kasi kwenye mitandao ya kijamii na vyombo vikubwa vya habari ndani na nje ya nchi.

Tangu wakati huo, hakuna tetesi yoyote ni wapi Dewji alipo huku Jeshi la Polisi likiwashikilia watu 12 kusaidia upelelezi wa tukio hilo lililotokea katika Hoteli ya Colloseum iliyopo Oysterbay jijini Dar es Salaam.

Kwa upande mwingine, tukio hilo limeamsha kumbukumbu na machungu ya matukio mengine kama hilo yaliyotokea miaka ya hivi karibuni yakiwamo ya kutekwa kwa watu mbalimbali kutoka kada tofauti.

Ni akina nani na wana nia gani?

Swali kubwa lililotawala kwa wananchi, ndugu wa Dewji na wadadisi wa mambo ni nani walio nyuma ya utekaji huo na kwa nini?

Nadharia zinazochambua kwa nini watu hutekeleza utekaji zimeorodhesha takriban sababu sita zinazoweza kumchochea mtu au kikundi cha watu kutekeleza utekaji ambazo ni pamoja na siasa, rushwa, tamaa ya utajiri, udini, ujinga pamoja na umaskini.

Je, ni ipi kati ya hizo inaweza kuhusishwa na kutekwa kwa mbunge huyo wa zamani wa Singida Mjini na mwekezaji katika klabu ya Simba? Kisiasa, Dewji aliwahi kuwa mbunge wa Singida Mjini kuanzia 2005 hadi 2015 alipoamua mwenyewe kutogombea.

Tangu wakati huo mfanyabiashara huyo amechagua njia ya kukaa mbali na siasa.

Vilevile hajawahi kutoa maoni ya kuunga mkono au kupingana na upande wowote wa kisiasa na amekuwa akitumia zaidi ukurasa wake wa Facebook na Twitter kutoa maoni ya kuhamasisha mafanikio ya biashara na jinsi ya kuzisimamia.

Je! ukimya wake huu wa kisiasa unaweza kuwa na nguvu ya kuwadhuru watu kisiasa kiasi cha kuwachochea kutekeleza utekaji huo? Hili ni swali linalodai majibu kutoka kwa wapelelezi wa tukio hilo.

Kwa upande mwingine, Dewji ni mfanyabiashara mkubwa anayemiliki zaidi ya kampuni 40 chini ya mwamvuli wa kampuni mama ya MeTL zinazofanya biashara katika nchi kadhaa za Afrika zikiwamo Kenya, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC), Malawi, Zambia na Sudan Kusini.

Pia, katika umri wa miaka 43 Dewji ametangazwa na Jarida la Forbes kuwa bilionea kijana kuliko wote barani Afrika akimiliki mali zinazokadiriwa kuwa na thamani ya Dola 1.3 bilioni za Marekani.

Utajiri wake unatokana zaidi na biashara za sekta mbalimbali na amefanikiwa kuliteka soko la bidhaa mbalimbali kiasi cha kushika miongoni mwa nafasi za juu kati ya kampuni binafsi zinazoongoza kwa kuajiri watu wengi nchini.

Hadi sasa hakuna tetesi yoyote kuwa shughuli zake za biashara zinaweza kumzalishia maadui kiasi cha kuamua kumteka.

Si rahisi pia kuzihusisha sababu za umaskini, tamaa ya utajiri na ujinga kwenye tukio la kutekwa Dewji.

Kwa nini Wazungu?

Juzi, kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa aliwaambia waandishi wa habari kuwa Dewji alitekwa na Wazungu wawili waliotoka katika gari aina ya Toyota Surf ndani ya uzio wa Hoteli ya Colloseum huku wakiwa wamefunika nyuso zao na kuondoka naye.

Hata hivyo, dereva wa Uber aliyeshuhudia tukio hilo alisema watu wanne walishuka kwenye gari dogo wakiwa wamejifunika usoni na kupiga risasi moja juu, hali iliyowakimbiza askari wa ulinzi hotelini hapo.

Tofauti na Mambosasa aliyedai watekaji walimchukua nje ya hoteli, dereva huyo alidai watekaji “waliingia ndani ya hoteli na kutoka na mtu ambaye nilimjua kuwa ni Mo Dewji.”

Taarifa za kuwa watekaji hao walikuwa Wazungu zimeibua shauku ya udadisi kama Dewji yuko katika mgogoro wa kibiashara na washirika wa kibiashara Wazungu.

Swali jingine linaloulizwa ni kwa nini Wazungu hao na hata watekaji wanaohusishwa na matukio yaliyopita wanawezaje kuendesha uhalifu wao ndani ya nchi na kutokomea mafichoni bila kujulikana.

“Nakwambia si rahisi kwa majambazi au wahalifu wa kawaida kuingia na kupanga utekaji kama huo na kutokomea kirahisi hivyo,” anasema mtaalamu mmoja wa masuala ya usalama aliyeomba kutotajwa jina.

Urahisi ambao watu wa aina hii wamekuwa wakitekeleza utekaji na kutoroka unaweza pia kuanika udhaifu wa utayari na uwezo wa vyombo vya usalama katika kuzuia uhalifu wa aina hiyo.

Hoteli ya Colloseum iko eneo la Oysterbay na kwa asili liko chini ya ulinzi wa kutosha kutokana na kuwa karibu na makazi ya viongozi wengi wa Serikali.

Kamera za usalama (CCTV)

Juzi Mambosasa alikataa kujibu moja kwa moja baadhi ya maswali ya waandishi akisema ni mapema mno kuyajibu na kutaka wapewe muda zaidi kufuatilia tukio hilo.

Hata hivyo, katika majibu yake kwa waandishi aligusia kuwa huenda tayari kukawa na ‘figisu’ zilizokwishafanyika kwenye kamera za usalama zilizotarajiwa kunasa namna utekaji huo ulivyotekelezwa.

“…na ndio maana tunawashikilia watu ambao kwa namna moja au nyingine wameshirikiana, haiwezekani mahali hapa watu wakaingia kirahisi namna hii,” alisema.

“CCTV kamera haionekani vizuri upande walipoingilia, kwa hiyo inaweza kuwa ni maandalizi ya kuweka mazingira ya watekaji.”

Walikuwa wakimtafuta siku nyingi?

Kuna taarifa iliyotolewa na dereva wake wakati akihojiwa na kituo kimoja cha redio kuwa inaashiria kuwa inawezekana watekaji wa Dewji walikuwa wanatekeleza mpango wa muda mrefu.

Dereva huyo anayemwendesha tangu mwaka 2011, alisema anamfahamu Dewji kama mtu anayeishi bila hofu dhidi ya raia, lakini akadai kuna kipindi takriban miezi minne iliyopita aliwahi kumgusia suala la tahadhari ya usalama.

“Kuna kipindi takriban miezi minne aliwahi kuniambia ‘bwana kwa sasa hivi tunapoelekea huko inabidi tuwe makini.’ Nikamuuliza kwa nini? Akaniambia kuna kipindi anapata meseji za vitisho,” alisema dereva huyo.

Nani atakomesha utekaji

Matukio ya watu maarufu kutekwa nchini yalianza kuripotiwa takriban miaka mitatu iliyopita pale msaidizi wa mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, Ben Saanane alipotoweka Novemba 28, mwaka 2016.

Tangu tukio hilo litokee, hakuna aliyekamatwa na hakuna tetesi Saanane yuko wapi na alitekwa na nani, ingawa Jeshi la Polisi linasema linaendelea na upelelezi.

Baadaye lilifuata tukio la kutekwa msanii wa Bongo Fleva, Ibrahim Musa maarufu Roma Mkatoliki aliyetoweka baada ya kudaiwa kutekwa Aprili, 2017, lakini alirejea nyumbani saa tisa usiku baada ya kutoonekana kwa siku tatu.

Hadi leo, Roma hajawahi kusimulia ni akina nani walimteka na walitaka nini kutoka kwake.

Julai 2017, mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibondo mkoani Kigoma, Simon Kanguye alitoweka na hajulikani aliko. Polisi wanadai kuwa alitekwa na watu wasiojulikana.

Tukio jingine lililotikisa nchi ni lile la mwandishi wa habari wa Mwananchi, Azory Gwanda aliyepotea tangu Novemba 21, 2017 nyumbani kwake Kibiti mkoani Pwani. Hadi sasa hajapatikana. Tangu matukio haya yaanze kutokea wabunge wa upinzani na wale wa chama tawala wamekuwa wakiitaka Serikali kufanya uchunguzi wa kina kuwabaini wahalifu hao ili kuepusha kuendelea kulitia doa Taifa.

Hata hivyo, kelele za wabunge, wanaharakati wa haki za binadamu na juhudi za Serikali havijafanikiwa kukomesha uhalifu huo.

Je, wanaotekeleza uhalifu huo ni mtu mmoja ama kikundi cha watu? Kinatekeleza uhalifu huo kutokea wapi? Wanapata wapi silaha na wanazitunza wapi?

Je, wana uwezo gani wa kuvikwepa vyombo vya dola kiasi cha kushindwa kukamatwa licha ya juhudi kubwa. Haya na mengine ni maswali ambayo majibu yake kila Mtanzania anayasubiri kama hakikisho la usalama wa raia.