Breaking News

Acacia kufutwa rasmi DSE leo

Monday November 18 2019

 

By Samuel Kamndaya, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Baada ya miaka minane ya kudumu katika Soko la Hisa Dar es Salaam (DSE), kampuni ya Acacia itafutwa rasmi kuanzia leo.

Kampuni hiyo, iliyoorodheshwa DSE Desemba 2011 ikijulikana kama African Barrick Gold (ABG) kabla haijabadili jina na kuitwa Acacia Novemba 2014, inaondolewa sokoni hapo baada ya kukamilisha utaratibu wa kufutwa.

“Acacia ilifutwa katika Soko la Hisa London (LSEG) tangu Septemba. DSE itaifuta kuanzia leo, Novemba 18, 2019,” inasomeka taarifa ya DSE iliyowekwa kwenye tovuti yake.

Kufutwa kwa kampuni hiyo, taarifa zinaonyesha kutapunguza ukubwa wa mtaji wa soko hilo kutoka Sh19.67 trilioni uliokuwapo mwishoni mwa wiki iliyopita hadi Sh16.94 trilioni.

Wakati ukubwa wa mtaji wa soko zima ukipungua, ule wa kampuni za ndani, Sh9.01 trilioni, hautabadilika.

“Hii inamaanisha ndio mwisho wa kuwa na kampuni ya Acacia katika soko letu. Walituandikia nasi tumewakubalia kuwafuta,” alisema Moremi Marwa alipozungumza na gazeti hili jana.

Advertisement

Kufutwa kwa kampuni hiyo ni utekelezaji wa taarifa ya Acacia kwa wadau wake Septemba 17 kuwa hisa zake zote zimenunuliwa na Barrick Gold Corporation.

Kabla ya mauzo hayo, Barrick ilikuwa inamiliki asilimia 63.9 na wanahisa wengine wakiwa na asilimia 36.1 zilizobaki.

Advertisement