Tigo yatangaza rasmi kuungana na Zantel

Monday November 4 2019

Mkurugenzi mtendaji was MIC Tanzania Simon

Mkurugenzi mtendaji was MIC Tanzania Simon Karikari 

Kampuni ya mawasiliano ya MIC Tanzania PLC (Tigo), leo imetangaza rasmi kuungana na kampuni ya Zanzibar Telecom PLC (Zantel) baada ya kukamilika kwa taratibu zote za kisheria na kiumiliki.

Taarifa iliyotolewa na Tigo inasema baada ya kupata vibali kutoka mamlaka zinazohusika, mchakato wa kuhamisha hisa na umiliki kamili kutoka Zantel kwenda Tigo umekwisha kamilika.

Kufuatia kukamilika kwa zoezi hili sasa makampuni haya yataunganisha shughuli zake za kiutendaji Tanzania Bara na Visiwani Zanzibar.

Akizungumza kuhusu muungano huo, Mkurugenzi Mkuu wa Tigo, Simon Karikari alisema hatua hiyo ina manufaa makubwa kwa Tanzania kwa ujumla.

 “Ninaamini kuwa kuunganishwa kwa kampuni hizi - Tigo na Zantel kutajenga huduma jumuishi kwa watanzania wote siku za usoni. Wateja wote wa Tigo na Zantel wataweza kufurahia huduma bora kutoka kwenye soko imara litakalosaidia kuchochea ubunifu kwenye sekta ya mawasiliano,” alisema Karikari.

Muunganiko wa makampuni haya mawili utasaidia katika kuimarisha utoaji wa huduma kwa wateja wa Tigo na Zantel waliopo kote Tanzania Bara na Visiwani.

Advertisement

Aliongeza: Aidha, muungano huu utawezesha kupanua wigo wa huduma zetu pamoja na kuongeza ubora wa upatikanaji wa mawasiliano katika maeneo ya mijini na vijijini. Vile vile muungano huu utasaidia katika usambazaji wa huduma za mawasiliano kwa makampuni na taasisi mbalimbali nchini na pia kupanua huduma za kifedha kwa njia ya simu za mkononi.

Karikari alisema wanategemea mafanikio chanya kutokana na muunganiko wa makampuni haya mawili wenye lengo la kuchangia kwenye maendeleo ya Taifa.

Zoezi la kuunganisha taratibu za kiutendaji wa makampuni zinatazamiwa kuanza hivi punde na wateja wa Tigo na Zantel wataendelea kupata huduma bila usumbufu wowote kutoka mtandao husika kwani namba na laini za wateja hazitabadilika.

Kampuni ya Mawasiliano ya Tigo ilianza kutoa huduma zake Tanzania tangu  mwaka 1995.

Advertisement