FFU wazingira ofisi za Tume ya uchaguzi kuzuia wagombea urais Uganda

Thursday January 9 2020Picha na Daily Monitor

Picha na Daily Monitor 

Kampala. Polisi wa kikosi cha kutuliza ghasia nchini Uganda leo wametanda makao makuu ya Tume ya uchaguzi (EC) ya nchi hiyo, saa chache kabla ya mkutano wa maofisa wa tume hiyo na wagombea urais.

Miongoni mwa wagombea urais ni Robert Kyagulanyi, maarufu Bobi Wine ambaye kwa siku za karibuni amekuwa tishio kwa Rais Yoweri Museveni, hasa miongoni mwa vijana.

Jumanne EC ilimwita mbunge huyo wa Kyadondo ikitaka kukutana naye kuhusu mikutano aliyopanga ya kura za maoni baada ya polisi kuzuia mikutano hiyo katika wilaya za Wakiso, Gulu na Lira, kwa madai ya kushindwa kukidhi masharti aliyopewa.

Kwa mujibu wa msemaji wa EC, Jotham Taremwa, mkutano huo unawalenga wagombea wote wa urais, tumewaita ili kujadili suala la mikutano yao ya maoni.

“Lengo la mkutano ni kuangalia namna ya kufanya mikutano ya maoni na kampeni. Kuwapo askari ni jambo la kawaida. Hakuna kitu cha ajabu,” amesema.

Novemba mwaka jana, kundi linalojiita ‘Serikali ya wananchi” linaloongozwa na Dk Kiiza Besigye liliishtaki EC likipinga uhalali wa mwenyekiti wake, Jaji Simon Byabakama, na katibu wake, Sam Rwakwojjo kuongoza tume hiyo kuelekea uchaguzi wa mwaka 2021.

Advertisement

Kundi hilo linadai kuwa Jaji Byabakama ambaye aliteuliwa mwenyekiti wa EC tangu Novemba 18, 2016, hajawahi kujiuzulu kazi yake kama Jaji wa Mahakama ya Katiba kama sheria inavyotaka, na kwamba kipindi cha pili cha Rwakojjo kilimalizika Septemba 19 mwaka jana.

Maofisa wa EC walitupilia mbali madai hayo wakisema hayana msingi kisheria na matumizi mabaya ya mahakama kwa kuwa maombi hayo yako nyuma ya muda na hivyo ni kinyume cha sheria.

 

Advertisement