ITIFAKI ILIPOWEKWA PEMBENI: Ruto alivyozuiwa uzinduzi wa BBI

Nairobi. Naibu Rais William Ruto alijikuta kwenye wakati mgumu kwa kuzuiwa nje na walinzi wa Rais Uhuru Kenyatta wakati wa uzinduzi wa ripoti ya Jopo la Maridhiano (BBI) kwenye ukumbi wa Bomas.

Ruto ambaye ndiye kiongozi wa pili kwenye serikali baada ya Rais, alizuiwa kuingia kwenye chumba cha wageni mashuhuri walimokuwamo Rais Uhuru, Kiongozi wa chama cha upinzani cha ODM, Raila Odinga na viongozi wengine.

Walinzi wa Rais Uhuru walimzuia Ruto kuingia kwenye chumba hicho na badala yake akatakiwa kusimama nje ya mlango asubiri mazungumzo yaliyokuwa ndani yaishe. Ripoti hiyo ilizinduliwa Jumatano iliyopita ya Novemba 27 na Rais Uhuru.

Kitendo hicho kimeelezwa kuwakasirisha baadhi ya watu kuona kiongozi wa haiba ya naibu rais kuzuiwa kuingia kwenye chumba hicho na badala yake kutakiwa kusimama nje ya mlango akisubiri mazungumzo yaliyokuwa ndani yaishe.

Walisema Ruto alidhalilishwa kwa njia ambayo haimfai yeyote wacha mtu wa kiwango cha Naibu Rais. Hali ya Ruto siku hiyo ilionyesha kuvunjika kwa uhusiano wa karibu kati yake na Rais Uhuru.

Baadhi ya wanaomuunga mkono Ruto walidai kitendo hicho kimewasha moto wa kisiasa ndani ya kambi ya kiongozi huyo.

Picha za video zilimuonyesha Ruto akiwa nje ya mlango huo huku mmoja wa walinzi akimzuia kuingia. Baada ya kuzuiwa Ruto alionekana akiwa hana furaha huku viongozi wenzake wengine aliokuwa nao nje walikuwa wakiendelea na mazungumzo.

Pia, ilielezwa kuwa Ruto hakujumuishwa moja kwa moja kwenye shughuli nyingi za uzinduzi wa ripoti hiyo katika Jumba la Bomas, jijini Nairobi licha ya juhudi zake kuonyesha umoja na ushirikiano kati yake na Rais Uhuru.

Baadaye Ruto aliungana na Rais Uhuru kwenye jukwaa, lakini sura yake ilionekana ya mtu asiye na furaha.

Licha ya Rais Uhuru kuonekana kufurahishwa na baadhi ya wazungumzaji, Ruto yeye hakuonyesha hisia zozote za kufurahishwa na kilichokuwa kikiendelea ukumbini.

Pia, viongozi wa tangatanga hawakuwa na nafasi ya kuzungumza kwenye hafla hiyo kiasi cha kuzua maswali ya iwapo kulikuwa na mpango wa kuzima sauti zao.