Ikulu yakataa kutoa ushirikiano kwa jopo la uchunguzi kumng’oa Trump

Wednesday October 9 2019

 

Washington, Marekani. Ikulu ya Marekani imesema haiko tayari kutoa ushirikiano kwa Tume ya uchunguzi dhidi ya madai yanayomkabili Rais Donald Trump.

Aidha, Ikulu imedai kuwa uchunguzi huo ni upuuzi na kwamba si halali kwa kuwa unakiuka Katiba ya nchi hiyo.

Awali Chama cha upinzani cha Democratic, kiliwasilisha barua katika ofisi hiyo kikitaka ushirikiano ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa muhimu zitakazosahidia uchunguiz huo.

Lakini jana Oktoba 8, Ikulu ya Marekani ilitoa tangazo hilo muda mfupi kabla ya Bunge la nchi hiyo halijamuhoji balozi wa Marekani katika Umoja wa Ulaya (EU), Gordon Sondland.

Katika barua iliyotumwa jana kwa viongozi wa Bunge hilo, mawakili wa Serikali ya Trump wameeleza wazi kwamba hawatoshiriki uchunguzi huo.

Hatua ya kukataa kushiriki katika uchunguzi huo inaonesha kuwa Trump sasa anaweza kuingia katika mvutano wa kikatiba na Bunge.

Advertisement

Sondland alitakiwa kutoa ushahidi wake jana mbele ya kamati za Bunge za kijasusi na masuala ya mambo ya nje.

Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge, Adam Schiff alisema kuwa uamuzi huo ni ushahidi mkubwa kwamba Trump na Waziri wa Mambo ya Nje, Mike Pompeo wamekuwa wakizuia uchunguzi huo.

Advertisement