Jimbo la California latangaza amri ya kukaa ndani kudhibiti corona

Muktasari:

Maambukizi ya virusi vya corona vimesababisha jimbo la corona nchini Marekeni kubaki nyumbani ili kujikinga na kuenea kwa maambukizi hayo yanayoenea kwa kasi dunia.

California. Jimbo la California nchini Marekani limewaamuru raia wake kukaa nyumbani ikiwa ni njia ya kudhibiti maambukizi ya virusi vya corona katika jimbo hilo maarufu zaidi nchini humo.

Kwa mujibu wa shirika la habari la BBC, Gavana wa jimbo hilo, Gavin Newsom amewaambia wakazi wa California kuwa watatakiwa kuondoka majumbani mwao tu wakati ni muhimu wakati wa mlipuko wa virusi vya corona.

Gavana huyo alikadiria kuwa zaidi ya watu milioni 40 katika jimbo lake wanaweza kupata maambukizi ya virusi vya Covid-19 ndani ya miezi miwili ijayo.

Tayari virusi vya corona vimeua watu 205 nchini Marekani huku watu wengine 14,000 wakipata maambukizi ya virusi hivyo.

Kwa ujumla wagonjwa karibu 250,000 duniani kote wameambukizwa virusi hivyo vinavyosabisha matatizo katika kupumua na takriban 9,900 wamepoteza maisha.

Gavana Newsom alisema “Wakati huu tunahitaji kuchukua maamuzi magumu.Tunahitaji kutambua hali halisi.”

Katazo  hilo litawaruhusu wakazi wa jimbo hilo kuondoka majumbani mwao kwenda kununua mahitaji ya nyumbani kama vile chakula au dawa. Hata hivyo, hawataruhusiwa kuwa kwenye mikusanyiko ya watu.

Pia, katazo hilo halitawahusu wafanyabiashara wanaofanya biashara za vyakula na bidhaa nyingine muhimu za nyumbani, maduka ya dawa, benki na vituo vya mafuta ya petrol. Biashara nyingine zitafungwa.

Takriban nusu ya wakazi wa jimbo hilo wameanza kutekeleza hatua hizo kali, likiwemo jiji la San Francisco.

Gavana Newsom amesema baadhi ya maeneo ya jimbo hilo yameshuhudia ongezeko la viwango vya maambuzi ya virusi vya corona mara dufu kwa kila baada ya siku nne.

Alielezea ubashiir wake katika barua kwa Rais Donald Trump Jumatano iliyopita, akitoa wito wa msaada wa haraka kutoka Serikali Kuu.

“Tunatazamia takriban asilimia 56 ya watu milioni 25.5 wataathiriwa na virusi vya corona katika kipindi cha wiki nane zijazo,” Gavana Newsom aliandika kama alivyonukuliwa na BBC.

Hadi sasa California imerekodi maambukizi ya corona yaliyo chini ya watu 1,000 na vifo 19 vya wananchi wake, hii ni kwa amujibu wa gazeti la Los Angeles Times.