Kimenuka tena Sudan; mamia waandamana kudai haki ya waliouawa

Muktasari:

Ni katika maandamano ya kumng’oa aliyekuwa Rais wa nchi hiyo, Omar al Bashir ambaye kwa sasa anashtakiwa kwa ufisadi.

Khartoum, Sudan. Mamia ya waandamanaji wamemiminika katika mitaa ya mji wa Khartoum kudai haki ya watu waliouawa kwenye maandamano dhidi ya Rais aliyeondolewa madarakani, Omar al-Bashir.

Waandamanaji hao walikusanyika katikati ya mji mkuu wa Khartoum na kuelekea ofisi ya Waziri Mkuu mpya, Abdalla Hamdok jana Jumamosi Novemba 30.

Kwa mujibu wa Shirika la habari la Ufaransa (AFP), waandamanaji hao wanadai mamlaka ya uongozi wa nchi hiyo kutoa haki kwa watu waliopoteza maisha ikiwa ni pamoja na kuwatafuta wote ambao bado hawajulikana walipo hadi sasa.

Waandamanaji hao wanadai kuna idadi kubwa ya wananchi wamepotea katika kipindi cha maandamano hayo.

Zaidi ya watu 250 wanaripotiwa kuuawa na wengine kadhaa kujeruhiwa wakati wa maandamano hayo yaliyosababisha kukomesha utawala wa Rais Omar al Bashir mwezi Dsemba mwaka jana.

Kiogozi huyo ambaye kwa sasa yuko gerezani akikabiliwa na tuhuma za ubadhilifu na kujipatia fedha isivyohalali alitawala Sudan kwa kipindi cha miaka 30.

Kufuatia hali hiyo Rais Bashir aliondolewa Jeshi katika mapinduzi ya Aprili 11 baada ya maandamano yaliyochochewa na mgogoro wa kiuchumi na hatimaye kuongoza nchi hiyo kwa mpito.

Hata hivyo, wananchi nchini humo waliandamana kwa miezi kadhaa kushinikiza utawala wa kiraia ambako zaidi ya watu 100 waliripotiwa kupoteza maisha.

Oktoba mwaka huu, uongozi huo wa jeshi ulikubaliana kushirikiana na raia katika kuunda Serikali kabla ya kuingia katika Uchaguzi Mkuu ambako wajumbe 11 wakiongozwa na kiongozi wa kijeshi uliapishwa kuivusha nchi hiyo katika kipindi hicho ambako nafasi ya waziri mkuu ilichukuliwa na raia.