Maandamano yang’oa Waziri Mkuu Iraq

Muktasari:

Ni simu moja baada ya waandamanaji 50 kuuawa kwa mpigo, huku mamia wakiwa wameshauawa tangu Oktoba.

Baghdad. Hatimaye Waziri Mkuu wa Iraq, Adel Abdul Mahdi amesema atawasilisha kwa Bunge barua yake ya kujiuzulu nafasi hiyo baada ya kutokea umwagaji mkubwa wa damu kwa waandamanaji wanaoipinga Serikali.

Uamuzi wa Mahdi ulitolewa katika taarifa yake leo Ijumaa umekuja baada ya wito wa kutaka mabadiliko ya uongozi wa juu wa nchi hiyo, uliotolewa na Kiongozi wa Madhehebu ya Shia nchini humo, Ayatollah Ali al-Sistani.

“Nitawasilisha barua ya kujiuzulu kwa Bunge kutoka wadhifa wa waziri mkuu ili Bunge liweze kufanya linachoweza kufanaya,” alisema.

Mapema leo Ijumaa, Al-Sistani amesema Bunge lililochagua serikali ya Mahdi yenye mwaka mmoja madarakani, linatakiwa kuangalia jambo la kufanya.

“Tunatoa wito kwa Bunge ambalo hii serikali ilitokea kuangalia namna ya kufanya kuhusu hili, Al-Sistani alisema katika mawaidha yake ya wiki katika mji mtakatifu wa Najaf, kupitia mwakilishi wake.

Abdul Mahdi amesema “nimesikiliza kwa umakini sana mawaidha ya Sistani na nimeamua kuitikia wito wake kwa kwa ukamilifu haraka iwezekanavyo.”

Hatua hiyo imekuja siku moja baada ya zaidi ya watu 50 kuuawa na vikosi vya serikali, siku ambayo ni ya umwagaji mkubwa wa damu, tangu maandamano ya kuipinga serikali yaanze mapema Oktoba.

Mamia ya watu wamekwishauawa na maelfu kujeruhiwa katika maandamano hayo huku vikosi vya serikali vikijibu mashambulizi kwa nguvu kubwa vikitumia mabomu ya macho ambayo yalielezwa kuwa na uzito kuliko ya kawaida.

Waandamanaji walikuwa wanalalamikia vitendo vya rushwa, ukosefu wa ajira na kudorora kwa huduma za jamii.