Breaking News

Marekani yasitisha ufadhili kwa shirika la afya duniani corona ikitajwa kuwa sababu

Wednesday April 15 2020

 

Washington. Rais wa Marekani, Donald Trump amesema Serikali ya nchi hiyo imesitisha ufadhili kwa Shirika la Afya duniani (WHO) kwa madai kuwa limeshindwa kusimamia mlipuko wa homa ya mapafu unayosababishwa na virusi vya wa corona.

Rais Trump amelishutumu shirika hilo kwa kutoweza kukabiliana na kusambaa kwa virusi hivyo  tangu vilipoanza mara ya kwanza huko Wuhan nchini China na kusambaa katika maeneo mengine ulimwenguni.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Uingereza (BBC), Trump  amesema shirika hilo linapaswa kulaumiwa kwa kuipendelea China wakati wote wa kukabiliana na janga la corona licha ya kuwa ugonjwa huo umesambaa katika mataifa mbalimbali.

Hata hivyo, Rais Trump mwenyewe anakosolewa nchini mwake kwa namna anavyokabiliana na mlipuko wa ugonjwa huo.

“Ninatoa mwongozo kwa utawala wangu kusitisha ufadhili wakati shirika hilo likiwa linachunguzwa katika majukumu yake iliyoshindwa kuyatimiza katika kukabiliana na usambaaji wa virusi vya corona,” Rais Trump aliwaambia waandishi katika Ikulu ya White House.

“Shirika la Afya Duniani (WHO) limeshindwa majukumu yake ya msingi na wanapaswa kuwajibishwa,” aliongeza Rais huyo wa Marekani.

Advertisement

Marekani ndiyo mfadhili mkubwa wa WHO na Taifa hilo linachangia kiasi cha Dola za Marekani 400 milioni ambayo ni sawa na asilimia 15 ya bajeti yake ya mwaka jana.

Mwaka 2018/19, China ilichangia karibu Dola za Marekani 76 milioni, kwa mujibu wa mtandao wa shirika la afya duniani.

 

 

Shirika hilo lilitenga kiasi cha Dola 675 milioni kwa ajili ya kukabiliana na magonjwa ya mlipuko na limeripotiwa kuwa litaongeza fedha hizo hadi karibu Dola bilioni moja.

“Mlipuko huu wa ugonjwa wa covid-19 unatia wasiwasi kama ukarimu wa Marekani umepewa kipaumbele sahihi au laa,” amesema Rais Trump.

Marekani ina idadi kubwa ya maambukizi ya virusi vya corona duniani kwa kuwa na wagonjwa 608,377 na vifo vilivyotokana na ugonjwa huo vimefikia 25,981.

“Hivi WHO imefanya kazi yake ipasavyo kwa kutumia wataalamu wake wa afya kuchunguza hali ilivyo China na kubaini ukosefu wa uwazi kwa kuwa kuna idadi ndogo ya vifo vilivyotokana na mlipuko huo.”

“Tukibaini hayo tutaweza kuokoa maisha ya maelfu ya watu na kuzuia uchumi wa dunia kuanguka. Lakini WHO iko tayari kuiamini China bila kuangalia uhalisia na kutetea hatua zinazochukuliwa na serikai ya China,” Rais Trump aliwaambia waandishi wa habari.

Siyo mara ya kwanza kwa jitihada za WHO kukosolewa katika namna wanavyokabiliana na janga hili, Februari mwaka huu, WHO ilisema katazo la kuzuia watu kusafiri halihitajiki ili kuzuia kusambaa kwa ugonjwa wa Covid-19, jambo ambalo lilipuuzwa na mataifa mengi.

Machi, shirika hilo lilishutumiwa kwa kushindwa kufanya majukumu yake baada ya maofisa wakuu wa China kukataa kwenda Taiwan kujadili namna ya kukabiliana na mlipuko wa ugonjwa huo.

Mji wa New York una visa 190,000 na zaidi ya vifo 10,000 vilivyotokana na ugonjwa wa corona, hata hivyo, kuna dalili ya maambukizi hayo kushuka.

 

 

Advertisement