Wananchi Rwanda wazuiwa kutoka nje kuepuka maambukizi ya corona

Muktasari:

  • Serikali ya Rwanda imetangaza zuio la watu kutoka nje huku ikiruhusu huduma muhimu kuendelea kutolewa katika kipindi ambacho Serikali inapambana kudhibiti maambukizi ya virusi vya corona.

Kigali. Serikali ya Rwanda imetangaza zuio la watu kutoka nje huku ikiruhusu huduma muhimu kuendelea kutolewa katika kipindi ambacho Serikali inapambana kudhibiti maambukizi ya virusi vya corona.

Jana Jumamosi Machi 21, 2020  Waziri Mkuu wa Rwanda, Edouard Ngirente alitangaza hatua mbalimbali zilizochukuliwa ikiwemo katazo la kutoka nje nchi nzima ili kudhibiti ugonjwa wa corona ambapo Rwanda ina watu 17 ambao tayari wamethibitika kuambukizwa virusi hivyo.

Waziri Mkuu alisema katika taarifa yake kwamba mipaka yote inayozunguka nchi hiyo itafungwa katika kipindi cha wiki mbili zijazo.

Hatua nyingine alibainisha kuwa ni kupiga marufuku safari zisizo za lazima katika miji na wilaya nchini humo wakati wafanyakazi wa umma na binafsi wakitakiwa kufanya kazi wakiwa majumbani mwao.

Wale wanaotoa huduma muhimu wataruhusiwa kutoka majumbani mwao na zuio la kukaa nyumbani halitawahusu.

Serikali ya Rwanda pia imepiga marufuku bodaboda kusafirisha abiria badala yake zitatumika kusafirisha vifaa mbalimbali.

“Mipaka imefungwa isipokuwa kwa mizigo na bidhaa pamoja na raia wa Rwanda wanaorejea nchini ambao watalazimika kukaa karantini kwa siku 14 mahali wanapofikia,” inasomeka sehemu ya taarifa ya Waziri Mkuu.

Pia, kutembea nje ya nyumba kumepigwa marufuku isipokuwa kwa huduma muhimu. Huduma za kifedha za kielektroniki zinahimizwa ili kupunguza mzunguko wa fedha za kawaida ambazo zinashikwa na kila mtu.

Hatua zote hizo, kwa mujibu wa serikali, zinalenga kudhibiti kuenea kwa virusi vya corona nchini humo.

 “Rwanda imechukua hatua kali kuzuia kuenea kwa mlipuko wa ugonjwa huu kama ilivyo katika mataifa mengine. Kama ni lazima, tutaongeza muda wa kukaa nyumbani kutoka wiki mbili za sasa,” alisema Waziri wa Mambo ya Nje wa Rwanda, Vincent Biruta.

Masoko na maduka yote yanayouza vyakula na bidhaa nyingine muhimu yataendelea kuwa wazi. Pia, hospitali, maduka ya dawa, vituo vya mafuta na usafiri wa umma zitaendelea kutoa huduma kama kawaida.

Hata hivyo, wasafirishaji watatakiwa kuzingatia tahadhari muhimu ikiwa ni pamoja na usafi na kuhakikisha abiria wanakaa angalau umbali wa mita moja kati yao.

Baa zote zitafungwa wakati migahawa itaendelea kuwa wazi lakini itakuwa ikiuza chakula na watu wanakwenda kulia majumbani kwao.

Waziri wa Afya wa Rwanda, Dk Daniel Agamije alieleza umuhimu wa kuzuia safari kati ya Kigali na miji mingine nchini Rwanda.

“Maambukizi mengi yamebainika hapa Kigali na hatutaki yaenee katika miji mingine hapa nchini kwa makundi ya watu wanaosafiri kutoka mji mmoja kwenda mwingine,” alisema Ngamije.

Zuio hilo limefuata hatua kadhaa ambazo serikali ya Rwanda imezichukua ikiwa ni pamoja na kufunga shule, makanisa na kuzuia mikutano na matukio yote ambayo yanawakutanisha watu wengi. Pia, waajiri walipewa maelekezo ya kuwaruhusu wafanyakazi wao kufanya kazi wakiwa majumbani mwao.

Mpaka kufikia Jumamosi, idadi ya maambukizi ilifikia 301,552 ulimwenguni kote wakati idadi ya vifo ikifikia 12,955. Shirika la Afya Duniani (WHO) limethibitisha kwamba watu 94,625 waliokuwa wameambukizwa ugonjwa huo wamepona.