‘ Mamlaka ya Mapato Tanzania iko tayari kuisaidia Uganda matumizi Stemp za kielektroniki ‘

Monday November 25 2019

Kaimu Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa

Kaimu Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi wa TRA, Richard Kayombo  

By Peter Elias, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imesema iko tayari kuisaidia Uganda katika mpango wake wa kuanza kutumia stempu za kodi za kielektroniki kama inavyofanyika nchini.

Kaimu Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi wa TRA, Richard Kayombo alisema juzi kwamba baada ya kujifunza kutoka kwa wengine, Tanzania iko tayari kuwasaidia Uganda na mataifa mengine kuachana na stempu za kawaida na kuanza kutumia za kielektroniki.

Kayombo alikuwa akizungumzia kauli ya Rais Yoweri Museveni aliyoitoa wiki iliyopita akiunga mkono matumizi ya stempu za kidigitali hata kwa bidhaa ambazo zinazalishwa Uganda.

Rais Museveni alikuwa akizungumza na mamlaka za kodi kutoka barani Afrika waliohudhuria mkutano wa usimamizi wa kodi Afrika uliofanyika Kampala wiki iliyopita na kusema hatua ya kuzisimamia kampuni za uzalishaji itasaidia kupunguza uvujaji.

Mkutano huo ulifanyika wakati Mamlaka ya Mapato ya Uganda (URA) ilipozindua mfumo wa matumizi ya stempu za kielektroniki Novemba Mosi, mradi ambao ulishuhudia watengenezaji wa bidhaa za soda, bia, maji ya chupa, sigara na pombe kali wakiweka stempu za kodi za kidigitali kwenye bidhaa zao.

Kayombo, ambaye alihudhuria mkutano huo nchini Uganda, amempongeza Rais Museveni kwa mtazamo wake.

Advertisement

“Kauli ya Rais inathibitisha kwamba uamuzi uliochukuliwa na Tanzania ambapo tulitimiza awamu ya kwanza kutoka Januari 15 kwenye bidhaa za pombe kali, mvinyo, bia na sigara wakati awamu ya pili ilianza Agosti Mosi, kwenye vinywaji laini kama maji na vinywaji vyenye kaboni,” alisema Kayombo.

Alisema wakati wote Tanzania iko tayari kubadilishana uzoefu na mamlaka nyingine za mapato, kwa sababu kwa kufanya hivyo, hiyo ni njia bora ya kujifunza kutoka kwa kila mmoja.

Kayombo alisema wamekuwa wakipokea wajumbe kutoka nchi mbalimbali ambao wanakuja Tanzania kujifunza kwa TRA juu ya mambo mbalimbali  kama vile Mashine za Kodi za Elektroniki (EFDs), makusanyo kwenye forodha na maendeleo ya ukusanyaji wa kodi ya pango.

“Mpaka sasa tumepokea ujumbe kutoka Botswana wakati Namibia nao wameomba kuja. Sisi pia tulijifunza kutoka kwa wengine kabla ya kuanza kutumia mfumo huo wa kodi. Tulikwenda Morocco, Malaysia, Uturuki na Kenya,” alisema.

Kayombo alisema jambo muhimu zaidi katika mfumo wa stempu za kielektroniki ni kuwezesha utunzaji wa kumbukumbu za uzalishaji na kiasi chake bila mtu yoyote kuingilia kati.

“Kwa njia hiyo, mfumo unahakikishia kodi stahiki inalipwa serikalini wakati ikiepusha pia migogoro isiyo ya lazima,” alisema.

Advertisement