Hoja ukomo wa ubunge yaibuka

Aliyekuwa katibu wa hayati Mwalimu Julius Nyerere, Samuel Kasori

Muktasari:

Msaidizi wa hayati Nyerere asema wabunge hawana uzalendo kwa kung’ang’ania kuwapo madarakani bila ukomo

Mbeya. Aliyekuwa katibu wa hayati Mwalimu Julius Nyerere, Samuel Kasori ametaka ukomo wa ubunge kama ilivyo kwa Rais.

Kasori aliibua hoja hiyo jijini Mbeya juzi wakati akiwasilisha hoja kuhusu dhana halisi ya uzalendo kwa Mtanzania katika mdahalo uliozungumzia ‘Uongozi wa kizalendo na maadili ni bora, kwa tathimini ya hapa tulipofikia’ ulioandaliwa na Serikali ya Wanafunzi wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUTSO).

Alisema ikiwa wabunge ndio walioweka ukomo wa Rais wa Tanzania ni miaka mitano, basi wanapaswa kuwaka ukomo wa kukaa bungeni.

Kasori alisema wabunge hawana uzalendo katika Taifa kwa kung’ang’ania kuwapo madarakani bila ukomo, wakati kuna Watanzania wengi wenye uwezo na nguvu ya kushika nafasi hizo.

“Inanikera na hii nazungumza kutoka moyoni. Tuseme ukweli, hawa hawa (wabunge) ndio wameweka ukomo kwa Rais. Kwa nini kule (bungeni) mpaka wafikie hatua ya kuzeeka,”? alisema Kasori.

Awali, Mkuu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), Waziri Mkuu mstaafu, Mizengo Pinda alisema ili kuuishi uzalendo, ni vyema mambo makuu manne yakatekelezwa na Serikali ikiwamo Taifa kutumia majeshi ya ulinzi na usalama kufundisha vijana dhana ya uzalendo.

Pia, alishauri kuelekeza nguvu katika shule za msingi na sekondari ili kuzalisha jamii au kizazi chenye uzalendo kwa nchi yao.

“Lakini kuanzia ngazi ya familia, wazazi watambue namna ya kumfundisha mtoto nini maana ya uzalendo. Pia, vyama vya siasa vitumike zaidi kueneza uzalendo na vijikite kwenye kujenga kambi maalumu zitakazofundisha uzalendo. Nimeona CCM wameanza hili, wamejenga chuo pale Ihemi-Iringa lakini na kule Pwani,” alisema Pinda.

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila alisema bado kuna viongozi wanataja zaidi uzalendo mdomoni lakini uhalisia hawayaishi matendo hayo.

“Tunamtaja sana Mwalimu Nyerere, tunawataja sana viongozi waliopita, lakini yale maisha halisi ya kumuishi baba wa Taifa hatuna kabisa,” alisema Chalamila.