Idris awagonganisha Makonda, Kigwangalla

Thursday October 31 2019
idriss pic

Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda jana alimtaka msanii wa vichekesho nchini, Idris Sultan kuripoti polisi baada ya kuweka picha yenye sura yake huku akiwa ameketi katika kiti chenye nembo ya Taifa.

Dakika chache baada ya Makonda kumtaka msanii huyo kuripoti polisi, Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamisi Kigwangalla alisema atamuwekea dhamana ikiwa ataripoti polisi na kukamatwa.

Katika ukurasa wa mtandao wa kijamii wa Instagram, Idris aliweka picha yenye sura yake akiwa ameketi katika kiti chenye nembo ya Taifa huku akiandika, “kwa siku moja tukabadilishana kazi ili a–enjoy siku yake ya kuzaliwa kwa amani.”

Baada ya kuweka picha hiyo, Makonda alichangia na kumtaka mchekeshaji huyo kwenda polisi.

“Naona mipaka ya kazi yako huijui, nenda sasa hivi kituo chochote cha polisi uwaambie Makonda kaniambia nije utakuta ujumbe wako,” alisema Makonda.

Baada ya mkuu huyo wa Mkoa kueleza hayo, Dk Kigwangalla aliandika katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Instagram, “nimeambiwa kuna msanii wa vichekesho anatafutwa na polisi.”

Advertisement

“Mniambie nitajitolea mwanasheria wa kwenda kumuwekea dhamana na kumtetea. Rais wetu ni mtu wa watu na imejidhihirisha kwa jinsi wananchi walivyojitolea kumuombea dua siku ya kuzaliwa kwake. Wameonesha upendo.”

Akizungumza na Mwananchi kuhusu Idris kwenda polisi, Makonda amesema, “nimesema kweli aende polisi sina utani na watu wa aina hiyo.”

Kuhusu hatua ya Dk Kigwangalla kumwekea dhamana Idris, Makonda alisema, “ Brother (kaka) ile Twitt sikumuandikia mtu yeyote zaidi ya Idris, nenda kaisome vizuri.”

Dokta Ulimwengu, meneja wa msanii huyo wa vichekesho alisema wamepokea wito wa Makonda na kwamba wanasheria wanashughulikia jambo hilo bila kufafanua watakwenda lini na kituo gani.

Baada ya Idris kuweka picha na maelezo hayo baadhi ya watu waliweka maoni yao akiwemo linexsundaymjeda, “unachokitafuta we jamaa.” Mwingine officialcassian aliandika, “dah tangulia central (kituo cha polisi kati) mwenyewe,” huku elizabethmichaelofficial akiandika, “ukoje.”

Advertisement