Madalali kubanwa, sasa watakiwa kuwa na leseni

Tuesday February 25 2020

Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Doto

Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Doto James. 

By Ephrahim Bahemu, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Serikali imetangaza mpango mpya ambao huenda ukapunguza idadi ya madalali baada ya kutaka kila anayefanya kazi hiyo na kunadisha kuwa na leseni kutoka wizara ya fedha.

Mpango huo unaoanza leo unawahusu madalali wa nyumba, viwanja na mashamba na wote wanaofanya shughuli kama hizo ambao wanatakiwa kukata leseni ambayo gharama yake ni Sh150,000 kwa mwaka.

Sharti hilo lilielezwa jana na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Doto James wakati wa uzinduzi wa mfumo wa kielektroniki wa utoaji leseni za udalali na uendeshaji wa minada.

James alisema kuanzia leo Serikali inaanza kuwashughulikia madalali na wanadishaji wasio na leseni kwa kusimamia utekelezaji wa sheria na kuzuia upotevu wa mapato.

“Tutakuwa wakali sana. Tumepoteza mapato mengi hata Serikali imewahi kuingizwa mkenge kwa kuwapa tenda watu ambao si rasmi, lakini sasa nisema madalali feki sasa hamtawaona tena mtaani, mtakutana nao Kisutu,” alisema James.

“Uzuri madalili wanafahamika na wengi wapo mitaani na wanajitangaza na mabango yao wameweka na mawasiliano, hususani Dar es Salaam, hivyo kwetu itakuwa ni rahisi kuwapata na kuwashughulikia.

Advertisement

Alisema hawatakuwa na huruma, watakuwa wakali kwa kuwa mapato mengi yamepotea.

“Madalali watakaokamatwa tutawatangaza katika vyombo vya habari, nitoe wito kwa wananchi wote na taasisi za Serikali kufanya kazi na madalali na wanadishaji wenye leseni,” alisema.

Kwa mujibu wa James, Serikali inakusudia kubadili sheria inayosimamia shughuli hizo kwa kuwa ile ya sasa ni ya takribani karne moja iliyopita (mwaka 1928) na ina mapungufu mengi ambayo hayaendani na mazingira ya sasa.

Mkurugenzi wa usimamizi wa mali za Serikali wa Wizara ya Fedha, Choto Sendo ambaye utoaji wa leseni uko chini yake alisema hadi mwaka 2019 jumla ya madalali na wanadishaji 136 ndiyo walikuwa na leseni na idadi yao imekuwa ikipungua mwaka mmoja hadi mwingine.

“Miaka ya nyuma walikuwa wengi kwa sababu vitu vya kuuzwa vilikuwa ni vingi lakini sasa wanapungua. Mfano mwaka 2017 waliokuwa na leseni walikuwa 186, 2018 wakawa 159 na mwaka 2018/19 wakawa 136,” alisema Sendo.

Kuhusu leseni kielektroniki, Sendo alisema huenda zikaongeza idadi ya wanaozimiliki kutokana na urahisi wa kuzipata bila kwenda wizarani.

Madalali na wanadishaji waliokuwepo katika uzinduzi huo walipongeza hatua hiyo wakisema inapunguza usumbufu wa kusafiri kwenda wizarani kufanya maombi ya leseni.

“Ni kweli kodi nyingi zilikuwa zinapotea kutokana na kuwepo kwa watu wengi wasio na leseni na sisi tupo tayari kuisaidia Serikali kuwabainisha. Pia leseni za kielektroniki ni nzuri na sasa mambo yote yatakuwa yanafanyika mkononi,” alisema Scholastika Kevela, mkurugenzi mtendaji wa Yono Auction Mart.

Advertisement