Breaking News

Mbatia, Komu wapinga kusimamishwa kampeni

Sunday October 18 2020

 

By Daniel Mjema, Mwananchi

Moshi. Mgombea ubunge Jimbo la Vunjo kwa tiketi ya NCCR-Mageuzi aliyesimamishwa kufanya kampeni kwa siku saba kwa madai ya kukiuka maadili, amegoma kutekeleza adhabu hiyo akisema hakitambui kikao kilichomhukumu.

Kikao kilichotoa hukumu hiyo, Mbatia amesema hakikuwa halali hivyo amewasilisha rufaa kwenye kamati ya Taifa ya maadili na wakati akisubiri uamuzi wa kamati hiyo, ataendelea na mikutano ya kampeni.

Katika barua ya mwenyekiti wa kamati ya maadili Jimbo la Vunjo, Michael Mwandezi ya Oktoba 16, kwenda kwa Mbatia, ilimjulisha kuwa kamati imemkuta na hatia hivyo atasimama kufanya kampeni kwa siku saba.

Wajumbe wa kamati hiyo walikutana Oktoba 16, baada ta kupokea tuhuma ya uvunjifu wa maadili dhidi ya Mbatia kwamba anatumia kipeperushi ambacho hakijaidhinishwa na msimamizi wa jimbo hilo.

“Kwa barua hii, kamati ya maadili imekukuta na hatia hivyo kukusimamisha kufanya kampeni kwa muda wa siku saba kuanzia Oktoba 17 hadi Oktoba 23,” inasomeka sehemu ya barua hiyo.

Mbatia ambaye ni mwenyekiti wa Taifa wa NCCR-Mageuzi, amethibitisha kukabidhiwa barua ya kusimamishwa kufanya kampeni.

Advertisement

“Ni kweli wamenisimamisha lakini nimeshangaa maana walipotaka nipeleke utetezi wa hicho kipeperushi tuliwapelekea na ushahidi wa barua iliyokitambulisha hicho kipeperushi. Tutatoa taarifa baadaye,” alisema.

Baadaye, meneja kampeni za NCCR-Mageuzi Jimbo la Vunjo, Hemed Msabaha alisema kipeperushi hicho kilipelekwa kwa msimamizi kwa barua yenye kumbumbuku namba HIM/Vol.36/2020 na ilipokelewa kwa dispatch.

“Kilichofanyika jana (juzi) sio kikao cha kamati ya maadili, kiliwahusisha watumishi wa uchaguzi na baadhi ya wajumbe wa kamati na hawakujadili bali walipiga kura kinyume cha taratibu,” alidai.

“Halafu kanuni zinataka aliyelalamika (CCM) na aliyelalamikiwa (NCCR-Mageuzi) wasishiriki kikao lakini CCM walishiriki. Kukiukwa huko kwa taratibu tunaona si kikao halali na tutaendelea na kampeni,” alieleza.

Msabaha alisema wameshawasilisha barua kwa mwenyekiti wa kamati ya kitaifa kutengua adhabu hiyo iliyotolewa na kikao kisicho halali.

Alipotafutwa Mwandezi ambaye ni msimamizi wa uchaguzi majimbo ya Moshi Mjini na Vijijini alipotafutwa jana hakupatikana kwani alikuwa katika kikao cha Tume ya Uchaguzi (NEC) na wasimamizi.

Kikao hicho kiliwajumuisha waratibu na wasimamizi wa uchaguzi wa mikoa ya Kilimanjaro, Arusha, Manyara na Tanga.

Wakati huohuo, mgombea ubunge Moshi Vijijini kupitia chama cha NCCR-Mageuzi, Anthony Komu naye amesimamishwa kufanya kampeni kwa siku saba kwa kukiuka maadili ya uchaguzi.

Mbali na adhabu hiyo, kamati ya maadili Jimbo la Moshi Vijini itakaa tena leo kujadili malalamiko mengine ya ukiukwaji maadili yaliyowasilishwa na mgombea ubunge wa CCM, Profesa Patrick Ndakidemi.

Komu anaingia katika orodha ya wabunge walioadhibiwa kutoendelea kufanya kampeni sambamba na mwenyekiti wake.
Wakati Komu akisimamishwa kwa kutumia bango ambalo halijaidhinishwa na msimamizi wa uchaguzi wa jimbo hilo, Mbatia yeye amesimamishwa kwa kutumia kipeperushi ambacho hakijaidhinishwa na msimamizi.

Jana Komu aliliambia gazeti hili kuwa amepewa adhabu hiyo lakini hajakubaliana nayo na anafanya mchakato wa kuwasilisha rufaa kwenye kamati ya kitaifa ya maadili ya uchaguzi mkuu.

Makosa mengine anayotuhumiwa nayo Komu yatakayosikilizwa leo ni wakala wake kuhudhuria mkutano wa mgombea wa CCM akiwa kwenye gari lenye picha za Komu.

Licha ya wagombea hao wa NCCR- Mageuzi, katika maeneo mengine wapinzani wameonja joto hilo akiwamo Maalim Seif Sharif Hamad wa ACT Wazalendo anayewania urais wa Zanzibar ambaye amesimamishwa kwa siku tano zikiwa ni siku chache baada ya mgombea urais wa Tanzania kupitia Chadema, Tundu Lissu kusimamishwa kwa siku saba.

Kwenye orodha hiyo, wamo wabunge na madiwani kutoka vyama tofauti vya upinzani.

Advertisement