Mchongo wa Diamond, Zuchu, Tuzo za Grammy uko hivi

Muktasari:

Kumbuka, kwa upande wa tuzo za muziki, Grammy ndizo tuzo kubwa na za heshima zaidi kwa mwanamuziki yoyote yule duniani kwa zaidi ya miaka 60 sasa tangu zilipoanza kutolewa kwake. Yaani kuanzia Jay Z, Drake, Ray C, Alikiba, Ruby, Nandy au Adelle mpaka Barnaba wote wanaota kupata tuzo hizi na kwa ambao wameshapata huenda bado wanaota kuvunja rekodi kwa kuzipata nyingi zaidi.

Mwanzoni mwa wiki hii wasanii watatu kutoka lebo ya muziki ya Wasafi walitajwa kwenye mbio za kuelekea kuwania tuzo kubwa zaidi za muziki duniani, Grammy. Wasanii hao ni Diamond Platnumz, Zuchu na Raymond Mwakyusa maarufu Rayvanny.

Kumbuka, kwa upande wa tuzo za muziki, Grammy ndizo tuzo kubwa na za heshima zaidi kwa mwanamuziki yoyote yule duniani kwa zaidi ya miaka 60 sasa tangu zilipoanza kutolewa kwake. Yaani kuanzia Jay Z, Drake, Ray C, Alikiba, Ruby, Nandy au Adelle mpaka Barnaba wote wanaota kupata tuzo hizi na kwa ambao wameshapata huenda bado wanaota kuvunja rekodi kwa kuzipata nyingi zaidi.

Sasa tuingie ndani kuzifahamu tuzo hizi kwa ukaribu pamoja na hatua waliyofikia watanzania wenzetu, Diamond, Zuchu na Rayvanny.

Kina Diamond Wapo hatua gani

Diamond na vijana wake wapo kwenye hatua ya mwanzo kabisa inayoitwa ‘consideration’. Hatua ambayo sio ya kubeza lakini kimsingi ni ya mwanzo sana na haina maana kubwa ikiwa msanii hatovuka kwenda hatua inayofuata.

Mshindi anapatikanaje

Mshindi wa tuzo hizi hupatikana kwa kupigiwa kura, lakini kura hizo hazipigwi na mashabiki kama ilivyo kawaida ya tuzo nyingi hususan za hapa Tanzania, bali kura za Grammy hupigiwa na ‘Academy’.

Iko hivi; waandaji wa tuzo hii ni jumuiya inayoitwa NARAS (Kwa kirefu chake National Academy of Arts and Sciences) ambayo kimsingi ni jumuiya ya wasanii wanaojihusisha na uandaaji wa muziki.

Tunaposema uandaaji tunamaanisha kuanzia kutengeneza beat, kuandika mashairi, kurekodi, kuimba, kutengeza video mpaka usambazaji wa muziki. Kwahiyo ndani ya jumuiya hii kuna wanachama zaidi ya 1000 ambao ndio wanakuwa wanapiga kura kuchagua nani ashinde.

Wanachama hao huwa ni watu wanaojihusisha na muziki kama vile waandishi, waimbaji na maprodyuza na hupata huo uanachama kwa kupendekezwa na watu ambao tayari ni wajumbe wa jumuiya hiyo.

Unafikaje Grammy

Ili kazi ya msanii yoyote iweze kushindania tuzo hizo, mmiliki wa kazi husika anatakiwa kutuma kazi zake kwa Grammy ikiwa ni pamoja na kipengele anachoomba kugombea. Yaani kama Diamond anadhani wimbo wake wa Jeje umekidhi vigezo atautuma pamoja na kuanisha anataka wimbo huo uwe kwenye kipengele gani.

Baada ya zoezi la kupokea kazi kumalizika, mamia ya kazi hizo hupitishwa kwa wataalamu ambao hufanya uthibitisho wa kwamba kila kazi inakidhi vigezo vya Grammy ikiwemo ubora na umiliki, lakini pia wataalamu hao wanaangalia kama msanii aliingiza kazi yake kwenye kipengele husika?

Yaani kama msanii aliomba wimbo wake uingizwe kwenye kipengele cha wimbo bora wa Hip Hop, wataalam wataangalia kwanza kama huo wimbo wenyewe ni Hip Hop kweli?

Halafu wataalamu hao huchuja nyimbo zote zilizotumwa na mwisho hubakiwa na idadi ya nyimbo tisa mpaka 30 kwenye kila kipengele, kisha huwapa nafasi wanachama wa Academy kupiga kura za awamu ya kwanza. (Diamond, Zuchu na Rayvanny ndiyo wapo katika hatua hii)

Lengo la upigaji kura wa awamu ya kwanza ni kuhakikisha kila kipengele kinabaki na nyimbo tano ambapo sasa nyimbo hizo ndio huhesabika kama ‘nominees’ wa tuzo za Grammy. Kiasi kwamba hata ikitokea msanii hajashinda, hupewa medali ya ushiriki ambayo ina thamani kubwa hasa kwenye suala zima la kujibrand.

Kwa sababu wasanii wote waliowahi kuchaguliwa kushiriki Grammy wanahesabika kama wasanii wakubwa duniani na thamani yao huwa juu.

Sasa, baada ya kubaki wasanii watano kwenye kila kipengele ndipo tena wanachama wa Academy hupewa nafasi ya kupiga kura kwa mara ya pili za kuamua nani awe mshindi. Na hapa wapigaji kura huimizwa kwamba kila mtu apige kura kwenye sekta aliyobobea.

Yaani kwa mfano, kama wewe ni mwandsihi wa nyimbo, ni vyema ukapiga kura kwenye kipengele cha mwandishi bora wa nyimbo kuliko kupiga kwenye kipengele cha video bora wakiamini kwamba utakuwa na uelewa zaidi wa uandishi kuliko uandaaji wa video.

Wasanii wa Afrika waliowahi kushinda Grammy

List ya wasanii wa Afrika waliowahi kushinda Grammy ni ndefu. Hata hivyo kwenye tuzo hizi cha muhimu zaidi sio tu kushinda, bali umeshinda katika kipengele gani kwani kuna baadhi ya vipengele vina taswira ya kwamba vipo kwa ajili ya wasanii wa Afrika.

Vipengele kama Albamu Bora ya Kiasili, mara zote hubebwa na wasanii au bendi au kwaya kutoka Afrika. Kwaya kama vile Soweto Gospel Choir na Ladysmith Black Mambazo ni miongoni mwa kwaya lilizowahi kushinda Grammy kupitia kipengele hicho.

Vipengele muhimu na vinavyotazamwa zaidi kwenye Grammy ni vinne na vinafahamika kwa jina maarufu la Big Four. Vipengele hivyo ni; Albamu Bora ya Mwaka, Rekodi Bora ya Mwaka, Wimbo Bora wa Mwaka na Msanii Bora Chipukizi, vipengele ambavyo tuzo zake kwa mwaka huu 2020 alizizoa zote Billie Eilish, msanii kutoka nchini Marekani.

Hata hivyo vipengele hivi ndivyo ambavyo mpaka sasa hakuna msanii kutoka Afrika aliyewahi kuvigusa.