Mifumo inavyowasumbua wananchi kwa kutoonana

Wakazi wa jiji la Dar es Salaam wakiwa kwenye foleni katika ofisi za Mamlaka ya Vitambulisho Vya Taifa (NIDA) zilizopo Kawe jijini jana, kwa ajili ya kujiandikisha ili wapate vitambulisho vya Taifa. Picha na Ericky Boniphace

Dar es Salaam. Peter Mushi, mkazi wa Dar es Salaam, anamiliki Kitambulisho cha Taifa, lakini amelazimika kurudi nyumbani Tegeta, nje ya Jiji la Dar es Salaam kufuata nyaraka zinazoweza kumsaidia kupata hati ya kusafiria.

Alikuwa ameenda makao makuu ya Idara ya Uhamiaji yaliyopo Kurasini akiwa na kitambulisho hicho pekee pamoja na barua ya ofisi yake kuthibitisha safari yake nje ya nchi.

Lakini ofisa wa uhamiaji alimtaka Mushi awasilishe nyaraka zinazotakiwa kisheria ili apewe pasipoti – cheti cha kuzaliwa au kiapo au kuthibitishwa kuwa raia kwa wageni.Nyaraka nyingine ni cheti cha kuzaliwa au kiapo cha wazazi, Kitambulisho cha Taifa na picha tano zilizochukuliwa kipindi cha maombi.

“Nilidhani kwa kuwa tayari taarifa hizo zimo katika kanzidata za Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida), ingekuwa rahisi kwao kuzipata kwa kuwa wako chini ya wizara moja,” alisema Mushi (si jina halisi).

“Nililazimika kurudi nyumbani Tegeta kuanza kusaka nyaraka nyingine ndio nikarudi kumalizia maombi yangu ya paspoti.”

Mushi ni mmoja wa Watanzania wengi wanaosumbuka katika kufuatilia hati ya kusafiria, bima ya afya, na huduma nyingine zinazohitaji utambulisho unaokubalika kiserikali.

Lengo la vitambulisho vya Taifa ilikuwa ni kurahisisha utambuzi wa wananchi kielektroniki na kuondoa usumbufu wa kutafuta taarifa kutoka sehemu tofauti, lakini hadi sasa bado kuna tatizo la mifumo ya idara za Serikali.

Na katika zama hizi za maendeleo ya teknolojia ya mawasiliano, kanzidata ya Nida inaweza kufikiwa kirahisi na mifumo ya idara tofauti za Serikali kujua utambulisho wa mwananchi anayehitaji huduma kama hati ya kusafiria, leseni ya udereva, bima ya afya, leseni ya biashara na kitambulisho hicho, nyaraka tatu kati ya hizo zikitolewa na Wizara ya Mambo ya Ndani.

Kwa mujibu wa Jaji Mkuu Ibrahim Juma, hata dhamana ya mahakamani ingeweza kuwa na ahueni kama Kitambulisho cha Taifa kingetumika badala ya mshtakiwa kutakiwa kuwa na barua kama za mfanyakazi serikalini au ofisa mtendaji wa kata.

Leseni ya udereva hutolewa na Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mapato (TRA) na moja ya masharti ni kuchukuliwa alama za vidole kielektroniki, kama ilivyo katika utoaji wa hati za kusafiria na Kitambulisho cha Taifa ambacho mahitaji yake ni makubwa zaidi.

Lakini kwa sasa hilo limekuwa tatizo kutokana na ama mifumo ya idara hiyo kutoonana au kutambuana, ama kutokuwepo na utashi wa viongozi wa taasisi kuunganisha mifumo yao ili huduma zipatikane kirahisi, kama benki zilivyoamua kutumia Kitambulisho cha Taifa au leseni za udereva kama nyaraka muhimu katika kumtambua mteja.

“Kitambulisho cha Taifa kinapaswa kuwa kila kitu katika suala la utambuzi wakati wa utoaji huduma zote,” anasema Edwin Bruno, mtaalamu wa Tehama na muasisi wa kampuni ya Smart Code.

“Endapo mifumo yote itaunganishwa na kuwa katika kanzi data moja, itarahisisha huduma nyingi na hilo linawezekana kwa kutumia (Application Programming Interface) APL.

“Baadaye wanaiweka hiyo public, yaani katika system nyingine ambazo zinataka kutumia mfumo wa kutambua mtu ili kumpatia huduma.

“Mfano anataka kuanzisha huduma fulani, badala ya kuanza kusajili watu upya, anaweza kuomba system yake ikaunganishwa na Nida kwa kutumia APL na watumiaji wakatumia moja kwa moja badala ya kujisajili tena.”

Lakini hali ni tofauti kwa taasisi hizo tatu za Serikali wakati wa kutoa nyaraka hizo-- hati za usafiria, kuendeshea gariama bima ya afya. Kila nyaraka ambayo mwananchi anaihitaji, atachukuliwa alama za vidole, utambulisho wake na kutakiwa kutoa nyaraka ambazo nyingi zilishafika Nida.

“Serikali inaona kuna haja ya kuweka mifumo ya taarifa za utambuzi pamoja. Na hivi sasa majadiliano yanaendelea ili kuona namna bora ya kufanikisha suala hilo,” alisema Waziri wa Mambo ya Ndani, George Simbachawene alipoulizwa na Mwananchi kuhusu mifumo ya idara hizo tatu kutowasiliana.

“Utaratibu wa kuweka data pamoja unafanyika nchi nyingine na unarahisisha mambo na kupunguza gharama za uendeshaji wa mifumo hiyo ya taarifa kwa kuwa na mfumo mmoja tu unaohudumia badala ya huduma kutolewa na mifumo mingi.

“Mimi kama waziri nayesimamia sehemu ya utambulisho wa uraia tu, naona umuhimu wa kuunganisha mifumo ya taarifa kama inavyofanyika nchi nyingine na majadiliano yanaendelea kuhusu lengo hilo ni kuhakikisha taarifa za utambuzi zinapatikana sehemu moja tu.

“Taasisi zote zinazohitaji taarifa za utambuzi zinaweza kupatikana Nida badala ya kila mtu kuwa na mfumo wake, isipokuwa Jeshi la Polisi kwa kuwa lazima liwe na mfumo wake kutokana na uchukuaji wao wa alama za vidole kuwa tofauti na wengine. Wao unazungusha kidole kizima.”

Lakini msemaji wa Idara ya Uhamiaji, Ally Mtanda alisema utaratibu wao unatokana na unyeti wa nyaraka wanayotoa.

“Ili kubadilika lazima Sheria ya Uraia na Sheria za Hati ya Kusafiria zibadilishwe,” alisema.

Alisema lengo la kutaka nyaraka za utambuzi ni kujiridhisha kuhusu uraia kwa kuwa dodoso la taasisi hizo mbili halifanani. Uhamiaji hupaswa kujiridhisha na nyaraka zinazowasilishwa.

“Si kwamba hatukiamini Kitambulisho cha Nida. Hapana, tunataka kujiridhisha na utanzania wa mtu na Nida wanatusaidia kujua utambuzi wa awali na baada ya hapo tunaendelea na utaratibu, sheria zinazotuongoza,” alisema.

Alisema lengo ni kudhibiti utoaji wa hati za kusafiria kwa watu hawastahili.

Mbali na idara hiyo, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) nayo haitumii taarifa za utambuzi zilizopo Nida katika kuandikisha wapigakura.

Mkurugenzi wa NEC, Dk Wilson Mahera alisema kwa sasa tatizo ni kwamba si Watanzania pekee wenye vitambulisho hivyo.

“Lakini mipango ya baadaye ni kuvitumia vitambulisho hivyo kwa kuwa Nida ndiyo itakuwa na kazi ya kutunza taarifa za Watanzania wote,” alisema Mahera.

Tayari TRA imeanza kutumia utambulisho wa Nida kupata taarifa, anasema mkurugenzi wa elimu kwa mlipakodi ya taasisi hiyo, Richard Kayombo.

“Kwa watu wenye utambulisho wa Nida kwetu hawahitaji tena kuchukua alama za vidole wala picha zao. Taarifa zao zote tunazipata Nida. Tumeanza tangu mwaka jana. Lakini kwa ambao hawana bado utaratibu ni kama wa zamani.”

Alisema suala hilo limewarahisishia kazi na kuongeza ufanisi wa TRA kwa kuwa watu hawahitaji tena kwenda ofisi zao kupata utambulisho wa namba ya mlipakodi bali wanapata wakiwa popote penye mtandao. Alisema hata usajili wa biashara sasa ni rahisi kwa kuwa mifumo hiyo imeunganishwa na Wakala wa Usajili wa Makampuni (Brela).