Taarifa Magufuli kukutana na viongozi wa CCM Ikulu yawa mjadala mitandaoni

Sunday January 19 2020

 

By Mwandishi Wetu, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Taarifa za Rais John Magufuli kuwaita viongozi wa CCM wa mikoa na wilaya kwa mazungumzo Ikulu jijini Dar es Salaam, zimezua mjadala kwenye baadhi ya mitandao ya jamii, huku baadhi ya viongozi wa CCM waliotafutwa kwa simu wakithibitisha kualikwa kuhudhuria mkutano huo.

Hata hivyo, baadhi ya viongozi waandamizi wa CCM waliopatikana walisita kuthibitisha kuwepo kwa mkutano huo, ambapo licha ya Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole kutumiwa barua hiyo kwa njia ya mtandao baada ya kuiomba lakini hakujibu chochote.

Naye Katibu wa Siasa na Uhusiano wa Kimataifa, Kanali Ngemela Lubinga alipotafutwa kwa simu, alisema hana taarifa kwa kuwa yuko safarini, huku akimtaka mwandishi kuandika kama alivyoona kwenye mitandao ya jamii.

Barua iliyosambaa katika baadhi ya mitandao ya jamii tangu juzi jioni, ilisema Januari 24, Rais Magufuli, ambaye ni Mwenyekiti wa CCM atakutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa chama hicho wa mikoa, wilaya na jumuiya zake Ikulu jijini Dar es Salaam.

Licha ya barua hiyo iliyotolewa na Torry Mkama ambaye ni katibu myeka wa katibu mkuu wa chama hicho, Dk Bashiru Ally, ikionyesha kutolewa Januari 17, 2019 katika maelezo yake imeonyesha wajumbe wote watakaoshiriki mkutano huo wanatakiwa kuwasili jijini humo Januari 23, 2020.

Jumla ya viongozi wapatao 800 wanatarajiwa kuhudhuria mkutano huo wakiwemo wenyeviti wa mikoa, makatibu wa mikoa, makatibu uenezi wa mikoa na pia viongozi hao kwa ngazi za wilaya.

Advertisement

Pia wenyeviti na makatibu wa jumuiya za chama hicho (wazazi, UWT na UVCCM) wa mikoa na wilaya zote wamealikwa,.

“Makatibu wote wa mikoa mnatakiwa kuanza maandalizi na kuwasilisha ofisi ya katibu mkuu orodha ya majina kamili, cheo na namba za simu za wajumbe wote kutoka katika mikoa yenu watakaothibitisha kushiriki ifikapo Januari 20 (kesho Jumatatu).

“Januari 24, saa 12.00 asubuhi wajumbe wote watakaoshiriki mazungumzo wanatakiwa wawe wamefika Ikulu. Katibu wa Mkoa unaombwa uwajulishe wajumbe wote ipasavyo,” inaeleza sehemu ya barua hiyo.

Baadhi ya wachangiaji kwenye mitandao ya jamii ukiwemo wa Twitter walikuwa na maoni tofauti wakihoji sababu ya mkutano huo wa chama kufanyikia Ikulu wakati chama hicho kinazo ofisi zake na kumbi za mikutano.

Miongoni mwao ni mchangiaji anayejitambulisha kwa jina la Kazaroho @Kazaroho3 akisema;

“CCM ina maana haina fedha ya kukodi ukumbi wa mikutano.”

Hata hivyo, mchangiaji anayejitambulisha kama Jay Boy @JayBoy10487471 alisema; “Sasa wewe ulitaka wafanyie kwako(?) CCM wanakumbi zao nyingi, wao ndio wenye mamlaka kwa sasa.”

Mchangiaji mwingine anayejitambulisha kama Ntobi naye alikosoa mkutano wa CCM kufanyikia Ikulu, akihoji; “Wamekosa ukumbi?”

Hata hivyo, hii si mara ya kwanza kwa CCM kufanyia mkutano Ikulu ya Dar es Salaam.

Akifungua mkutano wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM uliofanyika katika ukumbi wa Ikulu jijini Dar es Salaam Oktoba 2017, Rais Magufuli aliwakaribisha wajumbe hao akisema Ikulu ni mahali pa Watanzania wote.

“Kwa hiyo sioni aibu kuwakaribisha wana CCM, lakini pia hapa ni kwa Watanzania wote, na ndio maana kuna wageni kutoka nje wamefika hapa Ikulu, wanamuziki niliwakaribisha Ikulu, wakati wa futari tulifanyia hapa hapa. Kwa hiyo sioni ajabu ninyi kuwakaribisha hapa,” alisema Rais Magufuli.

Pia mara kadhaa vikao vya Kamati Kuu ya CCM vimekuwa vikifanyikia Ikulu jijini Dar es Salaam.

Tangu mfumo wa vyama vingi ulipoanza mwaka 1992, kwenye utawala wa awamu ya pili chini ya Ali Hassan Mwinyi vikao hivyo viliendelea kufanyikia Ikulu na utamaduni huo umeendelea kwenye utawala wa awamu ya tatu chini ya Benjamin Mkapa na hata awamu ya nne wakati wa uongozi wa Jakaya Kikwete.


Advertisement