Tusiruhusu Vitaya Tatu ya dunia

Thursday September 5 2019

 

By Saidi Nguba

Septemba 1 mwaka huu dunia imetimiza miaka 80 tangu kuanza Vita ya Pili ya Dunia. Ni muhimu kwa kizazi kipya kujua ukweli kuhusu vita hii vinginenvyo hakitajua hatari iliyopo mbele ya tishio la amani ya dunia.

Miaka sita ya vita hiyo (1939 – 1945) ilisababisha maafa makubwa kwa binadamu na watu zaidi ya milioni 60 kupoteza maisha. Ulipatikana ushindi dhidi ya ufashisti na ramani mpya ya kisiasa ya dunia ilichorwa na kutokea mabadiliko makubwa Afrika na Asia yaliyoharakisha mchakato wa kuutokomeza ukoloni katika mabara hayo mawili.

Takwimu katika taarifa na vitabu vya historia zinaonyesha kuwa jambo baya zaidi ni kuwa idadi kubwa ya waliokufa ni raia wa kawaida siyo wale waliokuwa katika medani ya vita. Majeshi yaliyohusika ni kutoka nchi 61, huku watu bilioni moja na milioni 700, asilimia 80 ya watu wote duniani wakati huo (waliokadiriwa kufikia bilioni 2 na milioni 100) walishika silaha.

Wanahistoria wanasema kuwa Vita Kuu ya Pili ya Dunia chimbuko lake ni Vita ya Kwanza ya Dunia (1914 to 1918) ambayo ilimalizika kwa kuacha mapigano kwa kupitia Mkataba wa Amani wa Versailles mwaka 1918 lakini siyo kwa kufikia amani kamili. Mwishoni mwa vita hiyo, Uingereza na Ufaransa ambao waliibuka washindi, hawakutaka kuachia walichokipata vitani na walioshindwa, Ujerumani, walitaka nao wasikose chochote kabisa.

Baada ya Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia, kuna tawala nyingi za kidikteta na kifashisti zilizochipuka Ulaya na kuwasha cheche za miali ya vita mpya. Shambulio lililofanywa na Italia iliyokuwa inatawaliwa kifashisti kwa Ethiopia mwaka 1935 na kushika madaraka kwa Jenerali Francisco Franco mwaka 1936 kulikosababisha vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Hispania ni miongoni mwa matukio ya awali yaliyochochea Vita Kuu ya Pili ya Dunia.

Sababu nyingine kuu iliyochangia ni kuzaliwa kwa Umoja wa Nchi za Kisoshalisti za Kisovieti (Union of Soviet Socialist Republics – USSR, au sasa Urusi, ambayo baada ya mabadiliko makubwa ya mwaka 1991 huko imechukua haki na majukumu yote ya Umoja wa nchi hizo). Kuzaliwa kwa USSR kulileta wasiwasi wa kuenea kwa siasa za Kisoshalisti duniani ambazo nchi za Ulaya Magharibi hazikuwa tayari kuziona zinanawiri. Katika hali hiyo pamoja na hali ngumu ya kiuchumi ya Ujerumani wakati huo baada ya Vita ya Kwanza ya Dunia, uongozi wa nchi nchini humo ukanyakuliwa na Chama cha Wafanyakazi cha Ujerumani (Nationalsozialistische Deutsche Arbeiterpartei NSDAP au Chama cha NAZI) kilichoongozwa na Adolf Hitler, mwaka 1933. Utawala wa Ki-NAZI wa Hitler uliweka lengo la kutaka kuitawala dunia, kwa njia yoyote ile. Ukaunda jeshi kubwa la kisasa lenye maguvu lakini pia ukaanzisha umoja wa nchi zilizokuwa zinafuata itikadi za kidikteta na kifashisti kwa kuzishirikisha Italia na Japan. Kwa upande mwingine, ili kukabiliana na umoja huo wa kifashisti, Uingereza, Ufaransa na Marekani, zikakubaliana kushirikiana kupambana nao.

Advertisement

Shabaha kuu ya Uingereza na Ufaransa ni kujihami dhidi ya uchokozi wa Ujerumani na kuona kwamba mashambulizi yoyote yatakayozuka yataelekea zaidi Mashariki mwa Ulaya na siyo Magharibi.

Septemba mwaka 1938, Uingereza, Ufaransa na Ujerumani ya Ma-NAZI, zilitiliana saini Mkataba wa Munich, ambao ulionekana kama vile ni kujaribu kuwaridhisha Wajerumani. Chini ya Mkataba huo Czechoslovakia ililazimishwa igawe sehemu ya nchi yake kwa Ujerumani. Lakini ilipofikia Machi, 1939, nchi yote ikachukuliwa na Ujerumani. Kilichofuata katika mikakati ya Hitler ni kuichukua Poland.

Jitihada za Urusi kuzishawishi Uingereza na Ufaransa zikubali kuwa na maafikiano ya pamoja na Urusi ya kujihami endapo patatokea na chokochoko na uchokozi wowote kutoka kwa Wajerumani hazikuzaa matunda. Mwanahistoria wa Kiingereza, Niall Campbell Ferguson, aliwahi kulizungumzia jambo hilo na kusema: “Wakati Warusi walipopendekeza kuwepo kwa mkataba wa pande tatu - Urusi, Uingereza na Ufaransa kujihami, siyo zenyewe tu bali pia na jirani zao kutokana na uchokozi wa Ujerumani, walikataliwa katu katu…”

rumani kwa kushirikiana na ya Italia yakaanzisha mashambulizi Kaskazini mwa Afrika na mwishoni mwa mwaka 1941 ilipangwa kuwa Mashariki ya Kati na India zichukuliwe kwa kushirikiana na majeshi ya Ujerumani na Japan.

Hata hivyo, wachambuzi wanasema hivi sasa dunia inashuhudia upotoshaji mkubwa kwa kupitia utaratibu wa kufanya “mapitio” ya kilichotokea kabla na wakati wa Vita Kuu ya Pili ya Dunia, kwa njia ya makala katika magazeti, vitabu, filamu na vipindi vya radio na televisheni. Warusi, walioathirika sana na vita hiyo na kupigana kishujaa kufa na kupona kuyafukuza majeshi ya kifashti wanayaona mapitio hayo ni upotoshaji. Vita Kuu ya Pili ya Dunia, wanahistoria wanasema, imetufunza mambo kadhaa, miongoni mwao ni kuwa, kwanza, tusiruhusu Vita ya Tatu ya Dunia kwa sababu haitokuwa na mshindi isipokuwa ustaarabu na maendeleo yaliyofikiwa duniani hivi sasa yatatoweka; tusiruhusu kuzuka kwa tawala za kidikteta.

Advertisement