VIDEO: Aliyekimbia kituo cha uangalizi maambukizi ya corona Dar akamatwa Iringa

Friday April 3 2020

By Mwandishi Wetu, Mwananchi [email protected]

Iringa. Jeshi la Polisi Mkoa wa Iringa limemkamata mtu mmoja  kwa madai ya kutoroka katika karantini jijini Dar es Salaam siku tatu tangu awasili Tanzania akitokea nchini Norway.

Akizungumzia taarifa za mtu huyo,  mkuu wa Wilaya ya Iringa, Richard Kasesela amesema alipata taarifa za kutoroka kwake kutoka kwa mkuu wa wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam, Daniel Chongolo na kuamua kumfuatilia.

“Nilipigiwa simu na Chongolo kwamba kuna mtu mmoja ametoroka na anaonekana yuko Iringa na tulichofanya tuliwasiliana na polisi, na kujua nyumba anayokaa na nikaongea na mganga mkuu wa hospitali yetu, ametoa wataalamu tumekuja tumemchukua na tumemuweka karantini.”

“Mtu huyu inasemekana alitoka Norway na ameingia Tanzania ana siku nne, alikaa  karantini siku tatu akatoroka,” amesema Kasesela.

Mkuu huyo wa wilaya amesema umakini unatakiwa kuwa mkubwa katika baadhi ya maeneo yenye karantini ili waliowekwa kwa ajili ya uangalizi wasiweze kutoroka.

“Kuna dalili sio nzuri hawa watu wanaachiwa achiwa huko katika karantini zetu, tuwe makini. Kuna mmoja alitoroka Tunduma na mpaka sasa hatujui yuko wapi. Mtu kukaa karantini si kwa nia mbaya ni nia njema kabisa.”

Advertisement

“Nyumba hii tumeiweka katika karantini na mganga mkuu atasimamia na kuwacheki wote wanaoishi katika eneo hili,” amesisitiza Kasesela.

Advertisement