Waandishi watakiwa kuchukua tahadhari ya usalama wao

Tuesday August 20 2019

 

By Gasper Andrew, Mwananchi

Singida. Waandishi wa habari mkoani Singida nchini Tanzania wametakiwa kuchukua tahadhari wakati wote ili kulinda usalama wao.

Tahadhari hiyo imetolewa mwishoni mwa wiki iliyopita na mwezeshaji na mwandishi mwandamizi mkoani Arusha, Mussa Juma wakati akitoa mada kuhusu usalama wa waandishi wa habari.

Mkutano huo uliandaliwa na Taasisi ya Waandishi wa Habari Kusini mwa Afrika (MISA Tanzania) kwa kushirikiana na Asasi ya Internews uliohudhuriwa na baadhi ya waandishi wa habari na wadau wa habari mkoani Singida.

Mussa alisema tunakoelekea kuna dalili za wazi  kuwa mazingira ya waandishi wa habari katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku yatakuwa magumu.

“Matukio ya kuuawa kwa mwenzetu Mwagosi  wa Iringa na kutekwa kwa Azory wa Pwani ni dalili tosha kwamba kazi ya uandishi wa habari ipo kwenye kipindi kigumu na cha  hatari kwa usalama wetu,” alisema mwezeshaji Mussa ambaye ni mwandishi mwandamizi kampuni ya mwananchi mkoa wa Arusha na kuongeza;

“Tutambue kwamba unapoandika au kutangaza habari baadhi ya watu wataifurahia. Pia wapo ambao hawataipenda. Hivyo unapaswa kujilinda au kujikinga wakati wote.”

Advertisement

Aidha, Mussa  amewataka waandishi kuhakikisha wanakuwa na bima wakati wote ili kujijengea mazingira mazuri ya kupata tiba hata asipokuwa na fedha.

Awali mwezeshaji  na mhariri wa kampuni ya Mwananchi,Tausi Mbow aliwataka wandishi wa habari kuzingatia maadili na sheria wakati wote, wanapokuwa wakitekeleza majukumu yao.

“Kutokujua sheria siyo kigezo cha kutouchukuliwa hatua, waandishi tuppende kujifunza na kuzisoma sheria mbalimbali zinazohusya masuala ya habari ili tufanye kazi bila kuvunja sheria za nchi,” alisisitza Tausi.

Afisa habari Halmashauri ya Mkalama, Omari Mtamike alisema utaratibu wa sasa wa utoaji tuzo mbalimbali kwa waandishi wa habari unahatarisha maisha ya  waandishi husika.

Akifafanua zaidi afisa huyo alisema habari inayopelekea mwandishi habari kupata tuzo wakati ikichapishwa kwenye gazeti haitataja jina itaandikwa imeandikwa na mwandishi wetu.

“Lakini siku ya tuzo ndipo majina ya mwandishi wa habari huyo yatatajwa na yeye ataonekana wazi. Endapo habari hiyo itakuwa imemjeruhi mtu, tamtambua mhusika aliyeandika habari hiyo. Kwa vyo vyote usalama wake utakuwa hatarini.

Hivyo, alishauri tuzo hizo zianze kutolewa ndani kwa ndani kwenye kampuni ya chombo anachofanyia kazi mwandishi anayeshinda tuzo husika.Utamaduni huo utamweka salama mwandishi wa habari husika.

Kwa upande wake mhariri wa radio Standard ya mjini Singida, Revocatus Phinias alitumia fursa hiyo kuliomba jeshi la polisi kutoa taarifa za matukio mbalimbali bila urasimu wa aina yo yote.

Naye Mrakibu mwandamizi wa jeshi la polisi Mkoa wa Singida, SSP Atubonyekisye Mwakalukwa aliwataka waandishi wa habari kuwa na subira pindi  wakiombwa wasubiri taratibu zisikamilishwe.


Advertisement