Maalim Seif atangaza mkakati wa uchaguzi mkuu 2020

Muktasari:

Aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF) nchini Tanzania, Maalim Seif Sharif Hamad ambaye sasa ni mshauri mkuu wa chama cha ACT-Wazalendo ametangaza maandalizi ya chama hicho kuelekea uchaguzi mkuu ujao mwaka 2020.

Unguja. Chama cha upinzani nchini Tanzania cha ACT Wazalendo kimetangaza mkakati wa maandalizi ya ilani itakayotumika katika uchaguzi mkuu mwaka 2020.

Hayo yamesemwa leo Alhamisi Novemba 21, 2019 na Mshauri mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad wakati akizungumza katika kongamano maalumu la kinamama wa chama hicho Vuga mjini Unguja, Zanzibar.

Amesema baadhi ya wajumbe wa chama hicho watapita kila kata kukusanya maoni ya wananchi kwa lengo la kuhakikisha wanatengeza sera bora zitakazoweza kukiuza chama hicho katika uchaguzi mkuu ujao.

Maalim Seif aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF) amesema ili chama kiwe na ilani bora na yenye kuwagusa wananchi ipo haja ya kuwashirikisha wananchi wenyewe kutoa maoni yao.

Amesema lengo kuu la kukusanya maoni ya wananchi ni kutaka kujua kwa undani zaidi yanayowakereketa wananchi hatimaye yawekwe kwenye ajenda zao ambazo watakwenda kuziunganisha  katika ilani ya uchaguzi  ya chama hicho.

Maalim Seif aliyewahi kugombea urais wa Zanzibar kupitia CUF amewataka vijana kutumia fursa za kikatiba kutoa maoni yao kinyume na kuvunja sheria za nchi ambapo anaamini maoni ya vijana yanaweza kusaidia kwa kiasi kikubwa kujenga nchi.