CUF waeleza mkakati ‘kutumia’ ofisi za ACT-Wazalendo Zanzibar

Wednesday December 4 2019

 

By Fortune Francis, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Siku chache baada ya mshauri mkuu wa ACT-Wazalendo, Maalim Seif Sharif Hamad kueleza njama za watu kuvamia ofisi za chama hicho ziliyopo Vuga mjini Unguja, chama cha CUF kimeibuka na kusema muda si mrefu kitaanza kuzitumia ofisi hizo.

Ofisi hizo zilikuwa zikitumiwa na CUF kabla ya Maalim Seif kukihama chama hicho na kujiunga na ACT-Wazalendo baada ya mahakama kumtambua Profesa Ibrahim Lipumba kuwa mwenyekiti wa CUF. Kwa sasa ACT ndio wanatumia ofisi hizo

Desemba 2, 2019 katika mkutano wake na waandishi wa habari, Maalim Seif alieleza kuhusu mpango huo, kwamba unaratibiwa na chama kimoja cha siasa.

Akizungumza leo Jumatano 4, 2019 mjumbe wa bodi ya wadhamini ya CUF, Musa Kombo amesema Desemba Mosi, 2019 chama hicho kilifanya ukaguzi wa ofisi zake zilizopo kisiwa cha Pemba wilaya ya Chakechake.

 

Kombo amesema kuna watu walivamia ofisi ya CUF iliyopo jimbo la Micheweni iliyojengwa na aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Shoka Khamis.

Advertisement

“Zipo ofisi nyingi za majimbo na matawi zilizojengwa kwa michango ya wabunge na wawakilishi wote waliokuwepo tangu  2005 hadi 2015 ambazo zimevamiwa na kubadilishwa rangi.”

“Chama kimoja cha siasa kinadai ofisi hizo sio za CUF, wanadai  tuliazimwa na waliokuwa wanachama wetu na sasa wanachama hao wamehamia kwenye hicho chama na wamekabidhi ofisi hizo na kuzipaka rangi,” amesema.

Mjumbe wa baraza kuu la uongozi Taifa la CUF, Nassor Amour amesema ibara ya 10(3) ya chama hicho inaeleza kuwa hata kama mtu akitoa mchango au mali anapofukuzwa au kuhama chama mali hizo zinabaki za chama.

"Tunaenda kuchukua ofisi zetu na matawi yetu pamoja na zoezi la upandishaji wa bendera litakalofanywa na Lipumba,” amesema Amour.

Advertisement