Bao la Mtibwa laondoka na MO Simba

Zanzibar. SIMANZI na hali ya sintofahamu imeanza kuingia pale Msimbazi. Ndio, Simba imepoteza taji la kwanza msimu huu baada ya kukubali kipigo cha bao 1-0 mbele ya Mtibwa Sugar, katika fainali ya Kombe la Mapinduzi.

Mchezo huo umepigwa jana usiku kwenye Uwanja wa Amaan mjini Zanzibar, ambapo Simba ikiwa na mastaa wake tegemeo ilionekana kuzidiwa kila idara na Mtibwa Sugar, ambao waliingia fainali baada ya kuichapa Yanga kwa mikwaju ya penati huku Simba nayo ikiwaondoa mabingwa watetezi, Azam FC.

Hata hivyo, wakati mashabiki na wapenzi wa Simba wakiugulia maumivu kwa kipigo hicho, mambo yamezidi kuharibika zaidi baada ya Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa klabu hiyo, Mohammed Dewji (Mo) kutangaza kuachia ngazi kutokana na kutoridhishwa na matokeo hayo.

Katika taarifa yake kupitia ukurasa wake wa Twitter muda mfupi baada ya kumalizika kwa mchezo huo, Mo alisema: “Baada ya kulipa mishahara inayofikia Sh4 bilioni kwa mwaka, najiuzulu wadhifa wa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi. Nitabaki kuwa mwekezaji na nitazingatia kukuza miundombinu ya soka la vijana.”

Mtibwa ambao walionekana kucheza soka safi na kumiliki mchezo huo, ilipata bao lake la ushindi dakika ya 38 kupitia kwa Awadh Salum, ambaye alipenya katikati ya msitu wa walinzi wa Simba.

 

Mchezo ilivyokuwa

Simba waliouanza mchezo huo kwa kasi na dakika ya 15 Meddie Kagere alichelewa kuunganisha krosi ya Gadiel Michel akiwa katika nafasi nzuri ya kufunga.

Dakika ya 16 Issa Rashid 'Baba Ubaya' alifanya kazi nzuri kutibua pasi ya Miraji Athuman aliyewachambua mabeki na kumtafuta Kagere, ambaye alikuwa katika nafasi ya kufunga kwa urahisi.

Simba waliendelea kuliandama lango la Mtibwa Sugar na dakika ya 21, Miraji alitengeneza nafasi nzuri lakini, shuti lake linapanguliwa na kipa Shaban Kado, ambaye jana alionekana kuwa imara langoni.

Dakika ya 23 Mtibwa walitulia na kutengeneza mashambulizi mazuri mawili kupitia kwa Japhary Kibaya, ambaye jana aliwasumbua walinzi wa Simba japo hakuwa makini kupachika mabao.

Pia, Mtibwa walifanya shambulizi lingine, ambapo shuti la Salum Kihimbwa liligonga mwamba na kutoka nje. Kama sio umahiri na utulivu wa kipa Beno Kakolanya, basi Mtibwa ingeweza kuondoka na ushindi mnono.

Dakika ya 24 Baba Ubaya alifanya kazi nzuri kuzuia shuti la Kagere na mpira kuwa wa kurushwa shambulizi lililotengenezwa na Clatous Chama aliyekimbia kwa ufundi akiwatoka wachezaji wa Mtibwa Sugar.

Dakika ya 34 Onesmo Mayaya alipotezea Mtibwa Sugar nafasi nzuri ya kupata bao baada ya kubaki yeye na Kakolanya, akishindwa kumalizia pasi ya Kibaya.

Simba walilazimika kufanya mabadiliko ya kwanza dakika ya 37 wakimuingiza Hassan Dilunga akichukua nafasi ya Miraji aliyepata maumivu na kutolewa nje.

Ilikuwa ni dakika ya 39 Mtibwa walifanikiwa kupata bao hilo kupitia kwa Salum kwa shuti rahisi akifanikisha kazi yake ya kuwatoka mabeki kisha kupewa pasi na Kihimbwa.

Dakika ya 43 Mtibwa walitengeneza shambulizi lingine kupitia Kibaya aliyewatoka mabeki wa Simba na kujikuta akienda chini, lakini mwamuzi Mfaume Nassor akakataa sio madhambi huku wachezaji wa Mtibwa wakilalamika kuwa penati.

Mpaka mapumziko Mtibwa walimaliza dakika 45 za kwanza wakiwa mbele kwa bao 1-0.

Kipindi cha pili Simba walirudi kwa kufanya mabadiliko mawili wakimtoa beki Tairone Santos na kuingia Pascal Wawa na Rashid Juma alitoka na nafasi yake kuchukuliwa na Francis Kahata.

Dakika ya 46, Chama aliingia ndani ya eneo la Mtibwa lakini, shuti lake lilipanguliwa na Kado na kuwa kona iliyokosa madhara.

Dakika ya 48 Mayaya alipoteza nafasi nyingine akiwa uso kwa uso na Kakolanya na shuti lake likapanguliwa.

Dakika ya 65 Ibrahim Ajibu aliyeingia dakika ya 60 akichukua nafasi ya Said Ndemla, alipoteza nafasi nzuri shuti lake kutoka nje ya lango la Mtibwa.

Dakika ya 67 Simba waliendelea kuliandama lango la Mtibwa wakitafuta bao la kusawazisha shuti kali la Ajibu linatoka pembeni kidogo chini ya lango la wapinzani wao.

Dakika ya 75 Simba walifanya shambulizi lingine zuri Ajibu akapaisha juu akiwa karibu na Kado, ambaye alifanya kazi kubwa ya kulinda lango.

 

Mo ang’oka Simba

Uamuzi wa Mo kuachia wadhifa huo Simba, umeibua sintofahamu sio kwa wanachama tu, bali kuhusu pia hatima ya bodi hiyo.

Habari za kuaminika zinaeleza kuwa, kwa Mo kuachia ngazi ina maana kwamba wajumbe waliobaki wanakosa uhalali wa kuendelea na wadhifa huo hivyo, bodi yote imepoteza sifa.

Hata hivyo, habari kutoka ndani ya Bodi hiyo zinaeleza kuwa ilitakiwa kuvunjwa muda mrefu kutokana na kuwepo kwa mgawanyiko ikiwemo baadhi ya wajumbe kususia vikao.

Awali, ilidaiwa kuwa aliyekuwa Mwenyekiti wa Simba aliyejiuzulu wadhifa huo, Swedi Mkwabi ndio chanzo cha mgawanyiko huo kutokana na kwenda tofauti na Mo.

Hata hivyo, kutokana na mgogoro huo Mkwabi aliamua kujiuzulu na nafasi yake kukaimiwa na Mwina Kaduguda.

 

Aussems akumbuka

 

Mara baada ya mchezo huo, mashabiki wa Simba ambao walionekana kukerwa na matokeo hayo, walianza kulimba jina la kocha Patrick Aussmes, ambaye alitimuliwa Simba kwa kile kilichoelezwa kuwa ni matokeo mabovu.

Mashabiki hao waliofurika kwenye Uwanja wa Amaan walikuwa wakiimba jina la Uchebe, ambalo alikuwa akiitwa kwa kutaniwa Aussems kutokana na staili yake ya kufuga mzuzu.