Advertisement

Aliyemnyonga mkewe afungwa miaka miwili

Friday October 23 2020
aliyemnyonga pic

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imemhukumu Yusuph Ismail (45), kifungo cha miaka miwili jela, baada ya kupatikana na hatia ya kumuua mkewe bila kukusudia.

Mahakama ya Kisutu imetoa hukumu hiyo baada ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, kutoa kibali ikae kama Mahakama Kuu kusikiliza kesi hiyo ya mauaji.

Ismail, mkazi wa Tegeta A alikuwa anakabiliwa na shtaka moja la kumuua mkewe, Maria au Magdalena Fabian baada ya kutokea ugomvi na wakati anatekeleza tukio hilo, mshtakiwa na mkewe walikuwa wamelewa.

Ismail alidaiwa kumuua mkewe kwa kumchapa na fimbo sehemu mbalimbali mwilini, kisha kumnyonga kwa madai ya kutokuwa mwaminifu kwenye ndoa yake.

Mpaka hukumu hiyo inatolewa jana, Ismail alikuwa amekaa gerezani miaka saba.

Akitoa hukumu hiyo jana, Hakimu Mkazi Kuu, Huruma Shaidi alisema mshtakiwa atatumikia kifungo cha miaka miaka miwili jela, baada ya kumtia hatiani kwa kosa la kuua bila kukusudia.

Advertisement

“Ninakuhukumu miaka miwili jela ili iwe fundisho kwa wengine, lakini kama hujaridhika una haki ya kukata rufaa.

Hakimu Shaidi alisema kwa kuzingatia mshtakiwa amekaa mahabusu tangu mwaka 2013, mahakama inampunguzia adhabu.

Kabla ya kutolewa hukumu hiyo, wakili wa Serikali, Ashura Mnzava aliomba mahakama kumpa mshitakiwa adhabu stahiki ili iwe fundisho kwa watu wengine ambao wanafanya ugomvi wakiwa wamelewa. Awali, mshtakiwa alikumbushwa shtaka lake na kukiri ndipo upande wa mashtaka walipomsomea maelezo ya awali.

Advertisement