Umoja wa Mataifa wazungumzia kukamatwa wapinzani, Serikali yajibu

Muktasari:

Kamishna wa Shirika la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa, Michelle Bachelet ameeleza kusikitishwa na taarifa za kukamatwa kwa viongozi wa vyama vya upinzani na wanachama wao nchini, baada ya kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu, akiitaka Serikali kuruhusu watu kuwa huru kueleza malalamiko yao.

Dar es Salaam. Kamishna wa Shirika la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa, Michelle Bachelet ameeleza kusikitishwa na taarifa za kukamatwa kwa viongozi wa vyama vya upinzani na wanachama wao nchini, baada ya kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu, akiitaka Serikali kuruhusu watu kuwa huru kueleza malalamiko yao.

Hata hivyo, katibu mkuu wa Wizara ya Sheria na Katiba, Profesa Sifuni Mchome alisema Serikali haijapata taarifa hiyo, na kueleza kuwa watu hao wamekamatwa kwa mujibu wa sheria.

Profesa Mchome alisema bado Serikali haijapata taarifa hiyo na kama ni madai ya watu kukamatwa ni kwa mujibu wa sheria.

“Inawezekana kweli wanaongelea Watanzania, lakini inaweza kuwa ni umbea,” alisema Profesa Mchome.

“Kama watu wamekamatwa ni kwa kuvunja sheria na kama amekamatwa kutakuwa na kitu wametuhumiwa na kama ni hivyo wana nafasi ya kujieleza, waliomkamata wakiridhika wanamwachia. Huo ndio utaratibu wa kisheria.”

Taarifa iliyotolewa katika tovuti ya shirika hilo la Umoja wa Mataifa jana inadai kuwa viongozi wa upinzani na wafuasi wao 150 wa Bara na Zanzibar wamekamatwa tangu Oktoba 27, siku moja kabla ya wananchi kupiga kura.

“Wakati baadhi yao wakiwa wameachiwa kwa dhamana, wengine bado wapo kizuizini,” ilieleza taarifa hiyo.

Taarifa hiyo inasema maofisa wa polisi wamethibitisha kukamata watu hao kwa madai kuwa walikuwa na mpango wa kufanya maandamano ya vurugu.

“Polisi walionya wananchi, Oktoba 31 kwamba hawataruhusu maandamano kufanyika, wakidai kuwa yangesababisha fujo na kutishia kuchukua hatua kali kwa ambaye angeshiriki maandamano hayo,” amesema Bachelet katika taarifa hiyo.

“Hali ya hatari nchini humo haitaisha kwa kuwanyamazisha watu hao wanaopinga matokeo ya uchaguzi, bali ni bora kuruhusu majadiliano ya pamoja,” . Kamishina huyo aliitaka Serikali kuwaachia huru watu waliokamatwa kwa kutekeleza haki yao ya binadamu na kuhakikisha ulinzi na utekelezaji wa sheria.

“Chini ya sheria kuna dhana ya kuwapendelea watu kwa kuamini kuwa watakusanyika kwa amani,” alisema Kamishna Bachelet.

Taarifa hiyo pia inasema licha ya kuwepo kwa ukamataji huo, pia wanasitikishwa na kubanwa kwa asasi za kiraia na waandishi wa habari na kuwepo kwa madai ya ukatili wa polisi kwa vyama vya upinzani wakati wa kuelekea Uchaguzi Mkuu.

“Bachelet ametaka kuwepo kwa uchunguzi wa kina na ulio huru kuhusu uvunjifu wa haki za binadamu wakati wa uchaguzi,” inaeleza taarifa hiyo.

Pia kamishna huyo alizungumzia suala la kufungwa mitandao ya kijamii na intaneti na kufuatilia habari za uchaguzi.

“Utoaji huru wa taarifa ni jambo la muhimu kwa jamii ya kidemokrasia hasa katika uchaguzi,” alisema Bachelet.