Aliyeachiwa kwa msamaha auawa akidaiwa kuua

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Revocatus Malimi 

Muktasari:

Mfungwa aliyeachiwa huru kwa msamaha wa Rais John Magufuli kutoka gereza la Bukoba mkoani Kagera anadaiwa kuua kisha na yeye kuuawa.

Bukoba. Mfungwa aliyeachiwa huru kwa msamaha wa Rais John Magufuli kutoka gereza la Bukoba mkoani Kagera anadaiwa kuua kisha na yeye kuuawa.

Kamanda wa polisi wa Mkoa huo, Revocatus Malimi amewaeleza waandishi wa habari jana kwamba mfungwa huyo alivamia stendi kuu ya mabasi juzi Desemba 13 na kumchoma mfungwa mwenzake kisu na kumsababishia kifo huku akiwajeruhi watu wengine watano.

 Amesema baada ya tukio hilo wananchi wenye hasira walimkamata na kumshushia kipigo hadi kupoteza maisha.

“Tukio hilo lilitokea saa tatu za usiku eneo la stendi kuu ya mabasi,” alisema

 Amesema kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo walidai kuwa ghafla mtu mmoja asiyefahamika majina yake mwenye umri kati ya miaka (30 hadi 35)  alivamia maeneo ya stendi hiyo na kumchoma kisu tumboni na usoni Godfrey Gobadi (35) dereva wa bajaji na kumsababishia kifo papo hapo ambaye pia aliachiwa kwa msamaha wa Rais.

 Amesema mtu huyo alizidi kusababisha hofu na taharuki kubwa kwa watu katika eneo hilo alipoendelea kuvamia na kuwachoma visu watu wengine na kujeruhi wananchi watano.

 Amewataja majeruhi kuwa ni Michael Bukerebe (26) mkazi wa Mwanza, Salum Athuman (35 ) mkazi wa Omukigusha Bukoba Jalia Abdi (40) mkazi wa Migera Bukoba, Jimmy Mashaeli (45), na Nasri Abdalah (19 ) mkazi wa Dar es Salaam.

 Amesema baada ya mtuhumiwa kufanya vitendo hivyo, wananchi wenye hasira kali walimvamia na kuanza kumshambulia na kumuumiza vibaya.

"Askari polisi waliokuwa doria na waliokuwa kituoni waliwahi katika tukio hilo na kufanikiwa kumuokoa mtuhumiwa asiendelee kushambuliwa lakini alifariki wakati akipelekwa hospitali,” amesema Kamanda Malimi.

 Amesema kwa mujibu wa karatasi iliyotolewa mfukoni mwa mtu aliyefariki kwa kuchomwa kisu ilikuwa na jina la (EX –CONV 655/2019 Godfrey Gobadi ndiyo iliyothibitisha kwamba alitolewa gerezani kwa msamaha wa Rais.

 Amesema mtuhumiwa aliyeuawa na wananchi hakuwa na kitambulisho chochote na alitambuliwa kwa asilimia 60 kuwa naye alitoka gereza la Bukoba kwa msamaha wa Rais na kwamba chanzo cha tukio hilo bado kinachunguzwa.

 Kaimu Mganga Mfawidhi wa hospitali ya Rufaa ya Bukoba mkoani Kagera Dk Mussa Sweya amekiri kupokea miili ya watu wawili na majeruhi watano Desemba 13 mwaka huu saa 3:30 usiku.

 Majeruhi wawili walitibiwa na kuruhusiwa kuondoka kutokana na kuwa na majeraha madogo na watatu walilazwa kwa ajili ya uangalizi wa karibu.