Aliyekuwa mgombea udiwani Chadema adai CCM ilimshawishi ajitoe

Friday October 23 2020

Serengeti.  Aliyekuwa mgombea udiwani wa Matare kupitia Chadema, Emmanuel Nyantori amedai kuwa alishawishiwa kujitoa katika kinyang’anyiro hicho na baadhi ya wafuasi wa CCM.

Katibu wa CCM Wilaya ya Serengeti,  Peter Mashenji alikanusha madai ya Nyantori, “awali  alishaniambia anapenda kuhamia CCM nikamkaribisha, baada ya muda akatimiza ahadi yake kwa madai ya kufurahishwa na sera, baadaye nikasikia madai kuwa ameshinikizwa nilimuuliza akakana kuwa hayo yanasemwa na wenzake tu.”

Oktoba 6, 2020 mgombea huyo aliandika barua na kuweka dole gumba kuwa amejitoa kisha akatoweka jimboni humo akidai alitishwa na baadhi ya makada wa CCM na kumlazimisha kusaini, huku taarifa zikidai kuwa alipokea fedha ajitoe.

Akizungumza na Mwananchi leo Ijumaa Oktoba 23, 2020, Nyantori amesema kwa sasa amehamia eneo la Shule ya Msingi Mugumu, Kata ya Stendi Kuu akihofia usalama wake kwa madai suala hilo limewachukiza wananchi.

"Oktoba 14 nilipoandaa mkutano wa kampeni Matare polisi wakanishusha kwa kuwa nilishajitoa, "amesema.

Hata hivyo , anakiri kusaini kujitoa pamoja na kuweka dole gumba  lakini akidai kulazimishwa.

Advertisement

Msimamizi wa Uchaguzi Serengeti, Juma Hamsini amesema ana barua za kujitoa na hatapigiwa kura.

Katibu wa Chadema Wilaya ya Serengeti, Julius Antony amesema suala la Nyantori kwa sasa hawahangaiki nalo kwa kuwa analalamika pembeni hafiki ofisini wala kwa msimamizi wa uchaguzi ili waweze kufuatilia.

 

Advertisement