Amuneke alishtaki shirikisho la soka Tanzania Fifa

Thursday September 12 2019

 Fainali za Afcon 2019, Stars, Senegal, Kenya na Algeria ,Emmanuel Amuneke ,Shirikisho la Soka Tanzania,TFF,

 

By Charles Abel

Kocha aliyeipeleka Tanzania kwenye Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) 2019, Emmanuel Amuneke aliyetimuliwa mara baada ya fainali hizo zilizofanyikia nchini Misri, amelishtaki Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa Shirikisho la mchezo huo  Duniani (FIFA) akilalamika kutolipwa stahiki zake.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na mitandao ya completesports.com na punching.com, Kocha huyo Mnigeria ameamua kupeleka shauri hilo FIFA ili waweze kulitatua.

"Nimewasiliana na FIFA juu ya hilo jambo. Sio suala la kupigia kelele, lakini nina imani watalitazama na kuamua kama ni sahihi mtu kutolipwa baada ya kufanya kazi," alisema Amuneke.

Amuneke aliyekuwepo hapa nchini tangu alipovunjiwa mkataba Julai mwaka huu, inadaiwa amerejea Hispania ambako ndiko makazi yake ya kudumu yalipo.

TFF walifikia uamuzi wa kuvunja mkataba na Amuneke baada ya Taifa Stars kufanya vibaya katika  fainali hizo za Afcon 2019 zilizofanyika kati ya Juni 21 hadi Julai 19.

Katika fainali hizo, Stars ilishika mkia kwenye kundi C lililokuwa pia na timu za Senegal, Kenya na Algeria baada ya kupoteza mechi zote tatu, ikiruhusu nyavu zake kutikiswa mara nane na yenyewe kufunga mawili.

Advertisement

Algeria ndio waliobeba taji hilo kwa kuifunga Senegal katika fainali kali.


Advertisement