Anayedaiwa kumuua mkewe, kumchoma moto ataka fedha zake kwenye simu

Muktasari:

Hamis Said (38) anayedaiwa kumuua mkewe, Naomi Marijani ameiomba Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kumpatia fedha zake zaidi ya Sh5 milioni zilizopo katika simu zake mbili za mkononi


Dar es Salaam. Hamis Said (38) anayedaiwa kumuua mkewe, Naomi Marijani ameiomba Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kumpatia fedha zake zaidi ya Sh5 milioni zilizopo katika simu zake mbili za mkononi.

Amesema simu hizo zipo kituo kikuu cha polisi, Dar es Salaam, ameomba fedha zitolewe kwa matumizi ya nyumbani kwake, kumlipia mwanaye ada.

Said ametoa ombi hilo leo Jumanne Agosti 27, 2019 mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Salum Ally.

Mtuhumiwa huyo ambaye wakati  akiingia na kutoka mahakamani alikuwa amefungwa pingu miguuni  huku akiwa ameficha uso wake kwa kitambaa chekundu, ametoa ombi hilo baada ya wakili wa Serikali, Wankyo Simon kuieleza mahakama hiyo kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika.

“Kesi imekuja kwa ajili ya kutajwa na upelelezi wake bado haujakamilika hivyo tunaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa,” amedai Simon.

Wakili Simon baada ya kueleza hayo, mshtakiwa alinyoosha mkono na kumueleza hakimu kuwa ana mambo mawili anataka kuyasema ambayo ni   nakala yake ya hati ya mashtaka na laini zake za simu.

Said aliomba apatiwe laini hizo kusaidia familia yake na ada na kusisitiza kuwa katika kituo hicho kuna simu zake nne, mbili ndio zenye kiasi hicho cha fedha.

"Mimi sitaki simu ila naomba nipatiwe laini zenye fedha ili  nimpatie ndugu yangu namba ya siri aweze kutoa fedha kwa ajili ya matumizi, ikiwezekana zitolewe mbele ya polisi,” amedai.

Hata hivyo, wakili Simon amedai hawawezi kumpatia laini hizo kwa kuwa simu zake ni sehemu ya ushahidi wa kesi hiyo.

Amesema kama anahitaji fedha hizo aandike barua ya malalamiko na kuipeleka kwa Mkurugenzi wa Mashtaka Tanzania ( DPP) na nakala  aipeleke kwa Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai nchini( DCI) huku hakimu Ally akimtaka mshtakiwa kufanya kile  alichoelezwa na upande wa mashtaka.

Baada ya kueleza hayo kesi hiyo iliahirishwa hadi Septemba 10, 2019 itakapotajwa tena huku mshtakiwa akirudishwa mahabusu.

Katika kesi ya msingi Said anakabiliwa na kesi ya mauaji namba 4/2019. Anadiwa kutenda kosa hilo  Mei 15, 2019 katika eneo la Geza Ulole Kigamboni Dar es Salaam baada ya kumuua Naomi.

Anadaiwa baada ya kufanya mauaji hayo alimchoma moto kwa kutumia magunia mawili ya mkaa na kuchukua majivu na kuyafukia shambani kwake.