Benki ya Exim kinara tuzo ya mwajiri bora 2019

Muktasari:

Tuzo hiyo ya mshindi wa jumla ya Mwajiri Bora kutoka ndani ya Tanzania mwaka 2019, ziliandaliwa na kutolewa na Chama cha Waajiri Tanzania (ATE) mwishoni mwa wiki.

Dar es Salaam. Benki ya Exim Tanzania imeendelea kuwa kinara kwenye Tuzo za Mwajiri Bora (EYA) za mwaka 2019 baada ya  kuitwaa kwa mara nyingine tena.

Mwaka 2018, benki hii ilitwaa tena tuzo hiyo.

Tuzo hiyo ya mshindi wa jumla ya mwajiri bora kutoka ndani ya Tanzania mwaka 2019, ziliandaliwa na kutolewa na Chama cha Waajiri Tanzania (ATE) mwishoni mwa wiki.

Mbali na tuzo hiyo, ilishuhudiwa pia benki hiyo ikiibuka kinara kwenye Tuzo ya mshindi wa jumla ya ushirikishaji mzuri wa wafanyakazi ya mwaka 2019 sambamba na kutangazwa kuwa miongoni mwa waajiri kumi bora hapa Tanzania kati ya waajiri 800 walioshiriki kuwania tuzo hiyo.

Hafla ya utoaji wa tuzo hizo ilishuhudiwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Ajira na Watu wenye Ulemavu) nchini Tanzania, Jenista Mhagama.

Akizungumza baada ya kupokea tuzo hizo hivi karibuni, Mkuu wa Idara ya Rasilimali watu wa benki hiyo, Frederick Kanga alisema tuzo hiyo ni kiashiria tosha mbele ya jamii kuhusiana na namna ilivyowekeza kwenye rasilimali watu,  hatua ambayo ina umuhimu mkubwa katika kufanikisha malengo yake.

“Tuzo zote hizo tatu ni heshima kubwa kwetu na ni matokeo ya uwekezaji wa muda mrefu ambao tumekuwa tukiufanya kwa rasilimali watu kwenye taasisi yetu katika kuwasaidia waweze kutoa mchango wao kiutendaji katika ubora tunaoutarajia na ikibidi zaidi ya matarajio,” alisema Kanga.

Alisema moja ya vipaumbele vya benki yao ni pamoja na kuwaandaa watendaji wake kwa kuwaongezea ujuzi unaowawezesha kuwa mbele ya wakati katika utendaji kazi huku lengo likiwa ni kuleta matokeo bora na yenye ubunifu mpya kwa wateja.

“Lengo ni kuifanya taasisi yetu iwe sehemu ambayo mfanyakazi anakuwa bora zaidi, mwenye mabadiliko na mwenye utofauti,’’ alisisitiza.

Katika tuzo hizo kwa mwaka 2019, zaidi ya waajili 800 kote nchini  walishiriki kuwania tuzo mbalimbali ikilinganishwa na idadi ya waajili 150 tu walioshiriki mwaka jana.

Kwa mujibu wa Kanga, benki hiyo imedhamiria kuandaa wafanyakazi wenye ushirikiano katika kuunda timu imara ya pamoja kwa kuandaa mazingira ambayo wafanyakazi hao watajihisi kuwa wanathaminiwa, wanashirikishwa sambamba na kupewa fursa ya kukua na kujiendeleza kitaaluma.