Bulaya akwamisha kesi ya kina Mbowe

Muktasari:

Leo Jumatatu Oktoba 7, 2019 Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imeshindwa kuanza kusikiliza utetezi wa viongozi tisa wa Chadema akiwemo mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe kutokana na mshtakiwa Ester Bulaya kuwa mgonjwa.

Dar es Salaam.  Leo Jumatatu Oktoba 7, 2019 Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imeshindwa kuanza kusikiliza utetezi wa viongozi tisa wa Chadema akiwemo mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe kutokana na mshtakiwa Ester Bulaya kuwa mgonjwa.

Hayo yameelezwa leo na wakili wa utetezi, Profesa Abdallah Safari mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba kuwa kesi ilipangwa kwa ajili ya kuanza utetezi lakini mdhamini wa Bulaya amewapa taarifa kuwa mbunge huyo wa Bunda ni mgonjwa na amelazwa Hospitali.

Baada ya Profesa Safari kutoa taarifa hiyo, Ndeshukuwa Tungaraza ambaye ni mdhamini wa Bulaya aliieleza mahakama hiyo kuwa mshtakiwa huyo amepewa siku tatu za mapumziko katika hospitali hiyo.

Profesa Safari amesema kutokana na Bulaya kutokuwepo mahakamani, hawawezi kuendelea na utetezi.

Baada ya kueleza hayo Hakimu Simba aliiahirisha Kesi hiyo hadi Oktoba 15, 17 na 18, 2019.

Washtakiwa hao wanaanza kutoa utetezi wao baada ya mashahidi  nane wa upande wa mashtaka kutoa ushahidi wao na mahakama kuwaona washtakiwa hayo wana kesi ya mujibu.

Mbali na Mbowe, washtakiwa wengine ni naibu katibu  Salum Mwalimu (Zanzibar) na John Mnyika (Bara); mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche; mbunge wa Kawe, Halima Mdee; mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa; Mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko na katibu Mkuu wa Chama hicho, Dk Vincent Mashinji.

Washtakiwa hao kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka 13 ikiwemo kula njama,  kufanya mkusanyiko wenye ghasia, kuhamasisha hisia za chuki, kushawishi hali ya kutoridhika, uchochezi na kushawishi utendaji jinai kati ya Februari 1 na 16, 2018, mjini Dar es Salaam.