Bunge la Tanzania sasa kidigitali zaidi

Spika wa Bunge Job Ndugaia,akionyesha Tablet wakati wa Kikao cha kwanza cha Mkutano wa Kumi na saba wa Bunge mjini Dodoma leo. Picha na Anthony Siame

Muktasari:

Taasisi zinazotaka kutoa huduma za semina kwa wabunge zimetakiwa kuwa na mtazamo wa kimtandao badala ya kutumia makaratasi

 

Dodoma. Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai amezitaka taasisi zote zinazotaka kutoa semina kwa wabunge, wajiandae kuzitoa kwa njia ya mtandao kwa kuwa wabunge wako mtandaoni.

Spika Ndugai ametoa kauli hiyo leo Jumanne Novemba 5, 2019 katika kikao cha kwanza cha mkutano wa 17 katika Bunge la 11.

Kiongozi huyo amesema Bunge limepiga hatua kwa kuwa na teknolojia ya kisasa zaidi kwa kuwa na mitandao ya pamoja na vifaa vya kisasa.

“Lakini nawaomba na taasisi zingine kuiga mfano wa bunge kwa kuja na teknolojia ya kisasa ili kupunguza Makaratasi, lakini taasisi zinazotaka kutoa semina kwa wabunge wajipange katika teknolojia hii,” amesema Ndugai.

Wabunge wote leo waliingia na vifaa vya kisasa thabiti na kila kitu kimetumwa humo, hivyo wabunge walikuwa wakifuatilia kwa njia ya mtandao.

Hata hivyo, Mawaziri walikuwa wakijibu maswali ya wabunge kwa kutumia karatasi za majibu badala ya kusoma kwenye tabiti (tablet) zao.