Chadema Pwani wakosoa ziara za Makonda kutokana na corona

Friday April 3 2020

 

By Asna Kaniki, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Kanda ya Pwani kimesema kitendo cha Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kufanya ziara zinasosababisha mikusanyiko ya watu ni kuliingiza jiji katika hatari ya kusambaa kwa virusi vya corona.
Akizungumza leo Ijumaa Aprili 3, 2020 katibu wa chama hicho kanda ya hiyo, Hemedi Alli amesema kinachohitajika sasa ni kutoa elimu kwa wananchi wajue mbinu mbalimbali za kujikinga na siyo kuhamasisha mikusanyiko wala ziara zisizokuwa za lazima.
“Hatuhitaji siasa katika suala hili, hatutakiwi kufanya mzaha pia, watu walikatazwa kufanya mikusanyiko isiyo ya lazima lakini bado Makonda anakusanya watu kwenye vituo mbalimbali vya daladala bila tahadhari kwa madai kuwa anahamasisha umakini katika kujikinga na corona jambo ambalo ni hatari,”amesema.
Ameshauri uwazi katika kuripoti visa vya corona ili wananchi waweze kuchukua tahadhari zaidi.
“Haitoshi tu kuambiwa mgonjwa kadhaa mgeni au mtanzania amebainika kuwa na corona bali tujue ameupata ugonjwa huo na maeneo gani ili kujua mlolongo mzima hii pia itasaidia katika kuchukua tahadhari zaidi,”ameongeza.

Advertisement