Chadema wajitoa

Dodoma/Dar. Chadema imejitoa katika uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 24 na kuahidi kutotoa ushirikiano kwa viongozi watakaotokana na uchaguzi huo.

Uamuzi huo ulitangazwa jana na mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe mara baada ya kikao cha kamati kuu ya chama hicho na wabunge jijini Dodoma.

Alisema uamuzi huo umetokana na figisufigisu zilizofanyika katika uchukuaji, urejeshaji wa fomu za kugombea na uteuzi wa wagombea.

“Katika mazingira hayo walilazimika kukaa viongozi wa chama baada ya vikao imeonekana ni busara kwa chama chetu kutobariki uchaguzi wa kihuni. Na sisi kuendelea kushiriki katika uchaguzi huu ni kuhalalisha ubatili,”alisema Mbowe.

Hata hivyo alipoombwa maoni yake na Mwananchi, Waziri wa Tamisemi, Selemani Jafo alishangazwa na uamuzi wa Chadema kujitoa katika uchaguzi huo.

“Ingawa ni haki yao, lakini nimeshangazwa na uamuzi wao kwa sababu kila kitu kipo wazi.Kanuni haijamfunga mtu yeyote kudai haki ya kukataa rufaa,” alisema Jafo.

“Kweli kuna fomu zina makosa katika ujazaji, lakini mchakato wa rufaa unaendelea hadi kesho (Novemba 9).Huenda leo baadhi ya uamuzi kwa wagombea waliokataa rufaa ungetolewa, lakini nashangaa kujitoa kwao,” alisema Jafo.

Hata hivyo, Mbowe alisema wao kama chama wameamua hawatashiriki uchaguzi huo na kutoa maelezo kwa viongozi pamoja na wagombea wote kusitisha shughuli hiyo.

“Waachane na kukata rufaa waachane na kuweka mapingamizi, hatuko tayari kubariki ubatili huu….Hatutajitoa katika ujenzi wa kidemokrasia kwa kujitoa katika uchaguzi huu.

Mbowe alisema katika vijiji 12,319 walisimamisha asilimia 85 sawa na wagombea 10,471 na kwa upande wa vitongoji walisimamisha wagombea asilimia 78 sawa na wagombea 50,218.

Alisema chama chake kilisimamisha asilimia 85 ya nafasi zote zinazogombewa wote vitongoji, mitaa na vijiji.

Mbowe alisema waliofanikiwa kuchukua fomu na kuzirudisha walikuwa ni asilimia 60 ya kati ya asilimia 85 waliochukua fomu.

“Maana yake asilimia 25 ya wagombea wetu walioteuliwa na chama walinyimwa fomu, wako wengine walitekwa na kunyang’anywa fomu zao, wako walioshikwa na vyombo vya usalama hususan polisi,” alisema.

Alisema kutokana na vitendo hivyo vya hujuma ikiwemo ofisi kufungwa na wengine kushindwa kurudisha fomu kutokana na ofisi kufungwa kwa vyama vya upinzani matokeo yake tukapoteza asilimia 25 ya wagombea walioandaliwa na chama.

“Asilimia 60 ya waliorudisha fomu, wengine wakapokewa kwa misingi tofauti wengine zikapokelewa bila kupigwa mihuri, wengine wakarudisha fomu hawakupewa nakala moja. Pakawepo mizengwe mbalimbali angalau asilimia 60 walirudisha fomu, uhuni mkubwa na uharamia ndio ulipofanyika,”alidai Mbowe..

Alisema kati ya asilimia 60 ya wagombea ambao walifanikiwa kuchukua na kurejesha fomu ni asilimia 9 tu ndio majina yao yalipitishwa na Serikali hadi kufikia jana.

Alisema vimefanyika vitendo vya dhuluma dhidi ya demokrasia na kwamba walianza kulalamika tangu walipoanza kuandaa kanuni na miongozo.

“Tumelalamika Tamisemi haiwezi kusimamia uchaguzi kwa sababu wao ni Serikali. Lakini kwa sababu hawana utamaduni wa kuheshimu malalamiko wanalazimisha kusimamia uchaguzi ili waweze kuchakachua,”alisema.

Alisema watu wao wengi walienguliwa kwa sababu za kitoto, za kihuni na kwamba kuna wagombea ambao majina yao yaliongezwa herufi ili kubadilishwa jina.

“Wapo ambao waliambiwa kuwa chama chako hakitambuliki, ni uhuni tu, ilipelekea wagombea wetu kushuka hadi asilimia tisa…Wagombea wetu wanashushwa na watendaji ambao wamepewa maelekezo na Serikali,” alisema.

Alisema mambo hayo yanafanywa na viongozi wa Serikali wakiwemo wakuu wa wilaya na kwamba maeneo mengine CCM hawakuwa na wagombea na hivyo kuwalazimisha wagombea wa vyama vyao.

Alisema kinachofanyika sio aibu kwa Serikali bali ni fedheha kwa Taifa zima na kwamba mataifa mengine yataiona nchi kama majuha kwa uchaguzi huo aliodai ni wa kihuni

Alisema kwa upande wa jiji la Dar es Salaam waliweka wagombea katika mitaa yote 570 lakini majina yaliyopitishwa na Serikali yalikuwa ni 24 tu.

“Lakini tunawaeleza wanachama wetu hatushiriki katika chaguzi hizi wote wajitoe na wasitambue viongozi wote watakaopatikana katika Serikali za vijijini, mitaa na vitongoji na hiyo ni hatua ya kwanza tusilaumiane,” alionya.

Alisema hawatamtambua wala kutoa ushirikiano kwa kiongozi yeyote atakayepatikana kupitia uchaguzi huo.

Mbowe alilalamika kuwa Jafo amewataka wagombea kwenda kukata rufaa katika kamati ambazo wenyeviti wake ni makatibu tawala wa wilaya na hakuna mjumbe yoyote kutoka vyama vya upinzani.

Alisema hawaamini taasisi yoyote ya Serikali inaweza kusimamia uchaguzi nchini kwa uhuru na kwamba njia pekee ya kujenga utengamano na kuwezesha kuwa na chaguzi za haki ni lazima iundwe Tume Huru ya Uchaguzi.

“Ujenzi wa demokrasia katika chama chetu utaendelea na tutafanya shughuli zetu kwa nguvu tutaelezana siku zinavyokwenda,” alisema Mbowe.