Chadema wamshangaa Sumaye

Wednesday December 4 2019

 

By Peter Elias, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimeshangazwa na kauli zilizotolewa na waziri mkuu mstaafu, Frederick Sumaye aliyetangaza kung’oka katika chama hicho na kueleza kasoro mbalimbali za uchaguzi wa uenyekiti Kanda ya Pwani.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumatano Desemba 4, 2019 mkurugenzi wa itikadi, uenezi, mawasiliano na mambo ya nje wa Chadema, John Mrema amesema ndio mara ya kwanza anayasikia malalamiko ya Sumaye na kuhoji sababu za kutotoa taarifa kuhusu masuala hayo.

Katika mkutano wake na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, Sumaye amesema si mwanachama tena wa Chadema huku akimuachia ujumbe mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe.

Sumaye ameeleza hayo katika mkutano huo alioutisha  jana Jumanne Desemba 3, 2019 akieleza kuwa atazungumzia masuala ya kisiasa na uchaguzi wa Chadema unaoendelea.

Kutangazwa kwa mkutano huo kuliibua hisia tofauti kutokana na Sumaye aliyekuwa waziri mkuu  mwaka 1995 hadi 2005 kupigiwa kura 48 za hapana kati ya 76 katika uchaguzi wa uenyekiti wa Chadema Kanda ya Pwani. Kulingana na taratibu za chama hicho uchaguzi huo utarudiwa. Pia Sumaye alikuwa akigombea uenyekiti wa Chadema Taifa.

Sumaye amesema kutokana na yaliyomtokea kwenye uchaguzi huo na yeye kuchukua fomu ya kuwania uenyekiti akipambana na Mbowe haoni haja ya kubaki katika chama hicho.

Advertisement

Amesema katika uchaguzi wa Kanda ya Pwani wajumbe wa mkutano walishawishiwa na baadhi ya viongozi walioshiriki kumchukulia fomu ili asishinde.

“Nimelazimika kwa kulazimishwa kujiondoa Chadema na kuanzia sasa si mwana Chadema na sijiungi na chama chochote cha siasa. Nitakuwa tayari kutumika na chama chochote ikiwamo Chadema.”

Akizungumzia kauli za waziri mkuu huyo mstaafu, Mrema amesema, “hatuna taarifa za makundi kwenye chama chetu labda kama yeye alikuwa na kundi.  Sumaye alikuwa mjumbe wa kamati kuu ya chama alikuwa na nafasi ya kutoa taarifa hiyo na kama kweli ipo ingefanyiwa kazi.”

Mrema amesema wamezipokea taarifa za Sumaye kuondoka Chadema na kama mwanachama yoyote ameacha pengo kwenye chama hicho,  kwamba watatafuta namna ya kuziba pengo hilo.

Kuhusu uchaguzi wa chama hicho unaoendelea, Mrema amesema katiba ya Chadema hairuhusu mgombea kupita bila kupingwa,  kama mgomba ni mmoja lazima apigiwe kura ya ndio au hapana.

Amesema katika kura hizo mbili mgombea anaweza kupigiwa kura yoyote na wanachama kulingana na matakwa yao.

Mrema amesema Sumaye si mwanachama wa kwanza kupigiwa kura ya hapana, akibainisha kuwa kuna mwanachama mwingine mkoani Ruvuma alipigiwa kura ya hapana.

“Sababu kubwa aliyoitoa kuhusu kuondoka kwake Chadema ni shinikizo kutoka kwa familia yake, kwa hiyo sasa anakwenda kupumzika na wajukuu. Sisi tunamtakia kila la heri katika maisha yake na mapumziko mema,” amesema Mrema.

Advertisement