Chato kufungwa taa za barabarani

Wednesday September 11 2019

 

By Mwandishi Wetu, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Chato mkoani Geita nchini Tanzania,  E.L Mwaiteleke ametangaza zabuni ya kufungwa kwa taa za barabarani zinazotumia umeme wa jua kwa mwaka wa fedha wa 2019/20.

Zabuni hiyo yenye namba LGA/039/2019/2020/SPSL/W/01 imetangazwa jana Jumanne Septemba 10, 2019 katika Gazeti la Daily News ikizitaka kampuni za ukandarasi zinazotaka kazi hiyo kupeleka nyaraka za maombi yao katika bodi ya zabuni ya halmashauri kuanzia Jumatatu hadi Ijumaa isipokuwa siku zisizo za kazi.

Tangazo hilo la zabuni limewataka waombaji wawe na sifa ya kuwa na vifaa vya kutosha kufanya kazi hiyo, uzoefu katika kazi hiyo na kuonyesha mwenendo wake wa fedha, cheti cha Bodi ya Usajili wa Wahandisi (CRB), ulipaji wa ada kati ya mwaka 2017 au 2018, leseni na namba ya mlipa kodi.

Tangazo hilo limeelekeza maombi ya zabuni hiyo kuandikwa kwa lugha ya Kiingereza na nyaraka nyinginezo zinatakiwa kupelekwa na waombaji wa zabuni kupitia anwani iliyotajwa katika tangazo hilo na inatakiwa kulipiwa Sh100,000 kupitia Benki ya NMB.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa Hifadhi ya Taifa ya Burigi- Chato Julai 9, 2019, Mbunge wa Chato ambaye pia ni Waziri wa Nishati, Dk Merdad Kalemani aliwataka wawekezaji kwenda wilayani humo akisema itakuwa miongoni kwa majiji makubwa nchini humo.

 

Advertisement

Advertisement