Dk Mwakyembe ataja mikakati Kiswahili kuwa lugha rasmi Afrika Mashariki

Muktasari:

Maadhimisho ya Kiswahili yanafanyika kwa siku tatu jijini Arusha yakiwakutanisha wanahabari, wanafunzi wa ndani na wageni  wanaosoma kozi za Kiswahili, wahadhili pamoja na wapenzi wa  Kiwahili kutoka nchi wanachama wa  Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Arusha. Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe amesema Tanzania imejipanga kukifanya Kiswahili kuwa lugha rasmi Afrika Mashariki.

Dk Mwakyembe ametoa kauli hiyo leo Alhamisi Septemba 12, 2019 katika maadhimisho ya kitaifa ya Kiswahili na utamaduni yaliyozinduliwa katika Chuo cha Maendeleo na Ushirikiano wa  Kimataifa (MS TCDC) jijini Arusha.

Amesema tayari Baraza la Mawaziri la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) limemaliza mkakati wa lugha hiyo kuwa rasmi katika nchi wanachama.

"Tayari baraza la  mawaziri limepitisha Kiswahili kuwa lugha rasmi ya jumuiya kinachosubiriwa ni baraka za wakuu wa  nchi," amesema Dk Mwakyembe.

Amebainisha kuwa Kiswahili kimekuwa na mwelekeo mpya duniani jambo lililoleta mwamko kukitumia kwa ajili ya kufikia malengo ya kuwa na Tanzania ya viwanda.

Katibu Mtendaji wa  Baraza la  Kiswahili la Taifa (Bakita), Dk Selemani Sewangi amesema tamasha la  Kiswahili limefanyika kwa mara ya kwanza kwa kushirikiana na sekta binafsi.

Amesema tangu mwaka 2007 tamasha hilo halikufanyika kutokana na changamoto mbalimbali, kuanzia sasa litakuwa likiadhimishwa kila mwaka.

"Awali tulikuwa tunaadhimisha siku ya Kiswahili. Imepita miaka takribani 11 tangu lifanyike," amesema Dk Sewangi.

Mwenyekiti wa bodi ya chuo hicho, Dk Servacus Likwelile amesema mpaka sasa wameshawapa mafunzo wanafunzi wa  Kiswahili 9,200 wanaofanya kazi sehemu mbalimbali duniani.