Dk Ndugulile atoa maagizo sakata la mtoto aliyekatwa kiganja

Naibu Waziri wa Afya, Dk Faustine Ndugulile
Muktasari:
Sakata la madai ya mama wa mtoto wa miezi mitano aliyekatwa kiganja limechukua sura mpya baada ya naibu Waziri wa Afya, Dk Faustine Ndugulile kutoa maagizo kuhusu suala hilo.
Dar es Salaam. Sakata la madai ya mama wa mtoto wa miezi mitano aliyekatwa kiganja limechukua sura mpya baada ya naibu Waziri wa Afya, Dk Faustine Ndugulile kutoa maagizo kuhusu suala hilo.
Dk Ndugulile ametoa wiki mbili kwa msajili wa baraza la madaktari la Tanganyika kushirikiana na Baraza la Wauguzi na Wakunga Tanzania kufuatilia ukweli kuhusu madai hayo.
Naibu waziri huyo ametoa maagizo hayo leo Alhamisi Septemba 12, 2019 mjini Dodoma.
“Nilitegemea baraza la madaktari muwe mmeanza uchunguzi, kwa hiyo nakupa maagizo kesi hiyo muanze kufuatilia na kama itathibitika ni uzembe waliohusika wachukuliwe hatua, ndani ya wiki mbili mtuletee majibu ili mimi na waziri (Ummu Mwalimu) tujue tunachukua hatua gani,” amesema Dk Ndugulile.
Septemba 7, 2019 ilisambaa video mitandaoni ikimuonyesha Yvona akilia na kuwalalamikia wauguzi wa hospitali ya Mwananyamala kusababisha mtoto wake akatwe kiganja.
Yvona alieleza kuwa alimzaa mtoto wake akiwa mzima lakini siku 10 baadaye alianza kuumwa hali iliyosababisha kurudishwa hospitalini kwa ajili ya matibabu.
Kwa mujibu wa Yvona yalifanyika makosa wakati wa kumuwekea mtoto wake dawa, kusababisha dawa kusambaa kwenye kiganja na kuanza kuoza.