Hamahama, wapinzani kubanwa vyatawala mkutano NCCR-Mageuzi

Wednesday February 19 2020

 

By Kelvin Matandiko, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam.  Mjadala wa wanasiasa kuhama vyama pamoja na hofu ya kufa kwa mfumo wa vyama vingi nchini Tanzania ndio mjadala katika mkutano wa Halmashauri Kuu Taifa ya Chama cha NCCR-Mageuzi unaofanyika leo Jumatano Februari 19, 2020 jijini Dar es Salaam.

Mkutano huo wa kikatiba chini ya wajumbe 69 kati ya 79,  umehusisha pia ugeni wa Mbunge wa Moshi Vijijini (Chadema),  Anthony Komu, huku kada wa Chadema, Boniface Mwabukusi akitangaza kujiunga na NCCR.

Kabla ya Komu kutoa neno, mwenyekiti wa NCCR, James Mbatia aliwaeleza waandishi wa habari na wajumbe wa mkutano huo kwamba ndoto za kuirejesha Tanzania katika mfumo wa chama kimoja hazitafanikiwa kamwe huku akiapa kutohama chama hicho na kujiunga CCM.

“Niwaambie kama wana ndoto za kuirejesha Tanzania kwenye mfumo wa chama kimoja abadani hawataweza, Na umri wangu huu, tumeteseka sana, nimenyimwa elimu nchi hii, nikaenda kusoma nje, halafu leo hii useme tunarudi chama kimoja. Abadani hatutakubali.“

“Halafu ifahamike sisi sio kisiwa. Hatutarudi mfumo wa chama kimoja, nawaambia wenye mamlaka na Tume ya  Taifa ya Uchaguzi (Nec) haiwezekani, yaani unilazimishe niende Lumumba kuvaa jezi za kijani Lumumba ndiyo tuelewane? Hapana, hapana. Wacha nisiseme zaidi,” amesema Mbatia.

Lumumba ni mtaa uliopo jijini Dar es Salaam ambako zipo ofisi ndogo za CCM.

Advertisement

Akizungumza kuhusu hoja ya kuua mfumo wa vyama vingi nchini, Mwabukusi amesema endapo Taifa litakubali kuua mfumo wa vyama vingi, kitakachofuata ni kuzalisha ugaidi.

“Nje ya vyama vingi watu wataanza kujieleza kwa shoka, panga kwa ubini wake, kwa hiyo bado tunahitajiana  ukitaka kuua mageuzi ni kutaka kuua tunu ya Taifa hili, unaweza kufuta majina ya vyama lakini si akili na fikra za mageuzi. Bila kujali Chadema, NCCR tunahitajiana.”

Akizungumzia tuhuma na madai ya muda ya kuhamia CCM, Komu amesema bado ni mwanachama wa Chadema na endapo ataamua kuondoka Chama hicho hatakuwa tayari kuingia CCM.

“Sina rekodi ya kuwa CCM kama ninavyofananishwa na wengine, mwaka 1988 ili uwe kiongozi wa chuoni UDSM (Chuo Kikuu Dar es Salaam) lazima upitishwe Lumumba lakini tulikataa, tukaingia kwenye uchaguzi na kushinda tukarejesha Duso, sasa inaitwa Daruso (Serikali ya Wanafunzi UDSM).”

“Sasa kama chama kikinishinda siendi Lumumba, kushindwa Chadema ni kawaida kwa sababu vyama siyo mama yetu kwa mfano Mbatia akitaka kwenda aende tuone NCCR kama chama hakitaendelea,” amesema Komu.

Ameongeza, “Profesa Ibrahim Lipumba aliondoka CUF mwaka  2015 lakini CUF ikaimarika. Dk Willbrod Slaa aliondoka Chadema mwaka 2015 ikaimarika zaidi, kwa hiyo vyama ni mali ya wanachama, wanachama ni roho ya vyama. Niwaambie watu wa Moshi kama Chadema kutanishinda, nguvu zangu nitazipeleka kwingine kuimarisha upinzani zaidi.”

Advertisement