Hotuba ya Mwalimu Nyerere: Huwezi kununua haki

Friday October 11 2019

 

Jumanne, Machi 14, 1995, Mwalimu Julius Nyerere alizungumza na waandishi wa habari kwenye ukumbi wa Tanzania Room katika Hoteli ya Kilimanjaro, jijini Dar es Salaam na kusema kuwa ingawa haiwezekani kumpata Rais asiye na kabila, hatutamkataa mtu kwa sababu ya kabila lake, wala hatutamchagua mtu kwa sababu ya kabila lake. Aliasa pia kuepukana na udini. Sasa endelea.

Huwezi kununua haki. Haki hainunuliwi. Thamani yake shilingi ngapi haki. Lakini sasa tumetikiswa. Ufa mmoja mkubwa. Rushwa ya Tanzania siku hizi haina aibu.

Tanzania natembeatembea nje. Kuna watu wanaoniheshimuheshimu kidogo nje. Huwa natembeatembea. Kuna watu wenye heshima zao wanadai kanchi haka kana heshima. Sasa kananuka. Kananuka.

Nazungumza habari ya kutokusanya kodi. Kutokusanya kodi, wala msifikiri…kutokusanya kodi ni sifa moja ya viserikali corrupt (rushwa) popote pale. Popote. Wala msifikiri ni Tanzania peke yake au Kenya peke yake, hata Italy pale. Italy serikali hii iliyoondoka hivi wana mzigo wa madeni. Hawatozi kodi.

Serikali corrupt popote haitozi kodi, inatumwa na wenye mali. Inawafanyia kazi wenye mali. Serikali corrupt imwambie nini mwenye mali …serikali corrupt haikusanyi kodi. Itabaki ikifukuzana na vijitu vidogo vidogo mabarabarani hivi tu basi.

Hii ni jambo, ni sheria kama ile ya kwanza niliyowaambieni. Mkianza ubaguzi mtaendelea moja kwa moja. Hamna mahali pa kusimama mnasema tunasimama hapa. Mkishakuwa corrupt mtaabudu wenye mali. Mimi ni Mkristu. Sijui Kuruani inasemaje. Lakini Msahafu wa Kikristo, Injili, ambayo na Waislamu wanaikubali. Nabii Issa, maneno yake mwenyewe, huwezi kutumikia mabwana wawili. Moja, fedha, nyingine, Mungu, haiwezekani. Utachagua katika wawili hao.

Advertisement

Anasema ukipewa wawili hao usitamani wote, Mungu na fedha, acha Waswahili na fedha. Mungu na fedha. Anasema Nabii Issa mwenyewe, Bwana Yesu, huwezi kuchagua vyote viwili. Huwezi kuvitumikia vyote viwili.

Aliendewa na kijana mmoja akamwambia Bwana Mkubwa ili niende peponi nifanyeje, Bwana Yesu akamwambia si sheria ziko kadha kadha, moja mbili, tatu, nne tano, sita, si unazijua. Akasema nazijua hizi nazitii tangu ujana wangu. Hizo zote nazijua tangu ujana wangu na naziheshimu.

Akamwambia vyema, kama hivyo ndivyo, sasa nenda kauze mali yako yoote halafu uje unifuate, lo lo lo! Kijana yule, kijana yule katoka pale amesononeka kweli kweli.

Baada ya kijana yule kutoka ndipo Yesu alipolitamka hilo. Anawaambia wafuasi wake wale, tajiri kwenda peponi ni vigumu zaidi kuliko ngamia kupita katika tundu la sindano.

Wakamwambia wale wafuasi wake, malofa, sijui ni kwa nini wanamuuliza, malofa. Walikuwa malofa watupu wale. Wanamwambia Bwana Mkubwa kama hivyo ndivyo nani atafika peponi. Bwana mkubwa kuwapa assurance (uthibitisho) akasema ah, lisilowezekana kwa binadamu, kwa Mungu linawezekana. Yesu anawaambia hawa, tajiri kufika mbinguni anafika kwa muujiza wa Mwenyezi Mungu.

Rushwa, sasa Tanzania inanuka kwa rushwa. Ufa mwingine tulioupata. Tunataka kiongozi anayejua hivyo. Ambaye atasema rushwa kwangu ni mwiko. Mwaminifu kabisa kabisa. Hawezi kugusa rushwa. Na wanamjua. Na watoa rushwa watamjua hivyo. Lakini hatutaki aishie hapo tu. Maana haitoshi wewe mwenyewe uwe mwaminifu. Mambo haya yana matatizo. Unaweza ukawa wewe mwenyewe ni mwaminifu kabisa kabisa. Safi kabisa. Lakini una pressure za ndugu zako una pressure za jamaa zako una pressure za rafiki zako.

Kwa hiyo si kwamba inatosha wewe uwe mwaminifu tu. lakini uwe na uwezo wa kuwaambia jamaa zako, na rafiki zako, kwa kauli ambayo wataiheshimu na wala hawatarudia tena: Ikulu ni mahali patakatifu (vigelegele).

Unawaambia jamaa zako na marafiki zako firmly (kwa uthabiti) kabisa, Ikulu ni mahala patakatifu. Mimi sikuchaguliwa na wananchi wa Tanzania kuja kupageuza kuwa pango la walanguzi. Ukishawaambia hivyo ndugu zako, na rafiki zako, na ikajulikana hivyo, mtu mwingine wala hakusogelei. Wala hakusogelei. Nafsi yake haimtumi.

Lakini sasa kwenye uchaguzi nasikia mtu anakuja na pesa. Uchaguzi wa mwaka huu (1995) utakuwa uchaguzi wa pesa. Zamani katika CCM na katika Tanu, tunapochagua candidate (mgombea) wetu, kama ana mali tunamuuliza hii mali umeipata wapi.

Mali ilikuwa disqualification (kizuizi), mwaka huu (1995) mali itakuwa ndiyo number one qualification (sifa ya kwanza). Wamezipata wapi. Huo tunadhani ni ufa wa tatu umeitikisa nchi. Umeitikisa. Na watu wanajua. Wote mnajua watu wanajua.

Nilianza kwa kusema tulikuwa na miiko ya uongozi. Kuna miiko ndani ya Azimio la Arusha. Ilikuwa ni sehemu ya Azimio la Arusha. Sasa Azimio la Arusha silisemei maana siku hizi kulisemea Azimio la Arusha bwana lazima uwe na moyo kama wa mwendawazimu hivi (kicheko). Kwa hiyo sithubutu. Lakini Azimio la Arusha lilikuwa na misingi mingine misafi sana. Narudia. Nalisoma. Ninalo. Natembea nalo. Natembea na vitabu viwili. Natembea na Biblia na Azimio la Arusha.

Nakasoma narudia, sijagundua pabovu. Ni Azimio la misingi ya utu. Kimoja kiliweka miiko ya uongozi. Viongozi wetu walikutana Zanzibar wakaona Azimio la Arusha halifai.

Wala hawakututangazia, hawakututangazia kwamba tumekutana Zanzibar tumeona Azimio la Arusha halifai, walikuja kimya kimya tukaona wanaanza kufanya mambo hayafanani na Azimio la Arusha sasa wenye akili tukajua ndiyo limekwisha hivyo. Vyema, wala mimi sipigi kelele sasa. Nasema Azimio la Arusha kwangu mimi muhimu, lakini muhimu zaidi ni Tanzania. Azimio la Arusha halina maneno.

Lakini lilikuwa lina miiko. Hakuna serikali popote duniani inaendeshwa bila miiko. Hakuna. Wamarekani wana miiko. Waingereza wana miiko. Wajerumani wana miiko. Wafaransa wana miiko. Wajapani wana miiko. Hakuna kusema unaweza kuendesha tu nchi hivi bila miiko. Juzi juzi tu Uingereza pale kuna waziri mmoja katimuliwa. Waziri mdogo hivi. Kwa nini? Kwa sababu kapita pembeni huku amepita na mama mmoja wa barabarani (kicheko). Waingereza wanasema wewe waziri mzima unapita pita na …oooh (kicheko).

Watu walipoanza kusema sema huyu waziri alimwandikia Waziri Mkuu barua ya ku-resign (kujiuzulu), Waziri Mkuu kwa jinsi alivyokasirika wala hakumjibu. Alichagua tu. Alichagua mtu wa badala yake basi, wala hakumjibu. Wana miiko ya maadili tu.

Ukipewa kazi ya nchi lazima ujiheshimu. Huwezi kupewa kazi ya nchi halafu unaishi kihuni huni. Uhuni mabarabara yako tele, nenda kafanye uhuni wako kule.

Kwa hiyo nchi zote zina miiko. Hapa sasa hatuna. Wameacha ya Arusha hawakuweka mingine. Wameacha miiko ya Arusha hawakuweka mingine. Sasa ni holela tu. Ovyo tu. Ovyo kabisa.

Sasa tunataka kiongozi wetu anayekerwa na hilo. Tunataka mtu ambaye hilo linamkera. Na akituambia kuwa linamkera tukimtazama usoni tuamini. Maana si mtu anakwambia linakera sana lakini ukimtazama huyu (kicheko kirefu).

Mwaka jana nilitembelea Marekani pale. Akanikaribisha kwenye chakula cha jioni Getrude Mongella. Akanikaribisha kwake. Kama mnavyofahamu yupo pale anafanya kazi ya akina mama…Akanikaribisha kwake akakaribisha na jamaa wengine.

Yuko mama mmoja anatoka Uganda. Katika mazungumzo yule mama ananiambia Mzee, mimi nilikuwa nafanya kazi katika jumuiya ya Afrika Mashariki. Na tulipokuwa katika jumuiya tulikuwa tunawajua Watanzania. Si lazima watuambie. Sisi wa Uganda tulikuwa tunajuana kwa makabila yetu. Wakenya walikuwa wanajuana kwa makabila yao. Watanzania hatujui makabila yao hata kidogo.

Ilikuwa ni tofauti ya wazi kabisa. Sisi tunasemana kwa makabila, Kenya wanasemana kwa makabila, unajua huyu ni Mjaluo, unajua huyu Mkikuyu unajua huyu sijui ni Mnandi. Watanzania hapana. Ni Watanzania tu basi.

Na nilipokuwa nikiwashawishi Kenyatta na Obote tuunganishe nchi za Afrika Mashariki, safari moja tumekaa Nairobi nawaambia hivyo hivyo ninyi mna matatizo ya makabila…Na ninyi Kenya na Uganda mna matatizo ya makabila. Sisi hatuna.

Tukiungana hivi. Nchi hizi zikawa moja. Ukabila wa Kenya utapungua. Ukabila wa Uganda utapungua. Kwa nini. Kwa sababu katika nchi moja hivi ya East Africa, Wakenya mtajiita Wakenya mkitutazama hivi Watanzania mkaanza kuzungumza matatizo yenu, sasa mnasema mna matatizo mtamtafuta mchawi.

Mchawi yule mtamtafuta kwa Watanzania au kwa Waganda. Ninyi mtajiita Wakenya. Hamtayatafuta kwa Wakikuyu na Wajaluo. Hamtajibagua hivyo. Ndani ya federation (shirikisho) hamwezi kujibagua hivyo mkajiita sisi Wakikuyu, sisi Wanandi, sisi Wameru. Mtakuwa sisi Wakenya mbona Watanzania hawa wanatuoneaonea, wao wanapata mambo sisi hatupati.

Mtakuwa Wakenya ndani ya Muungano. Na Waganda mtakuwa hivyo hivyo. Mtakuwa Waganda ndani ya Muungano. Na Watanzania tutaendelea kuwa Watanzania hivyo. Lakini kwenu ninyi ukabila utapungua. Uganda utapungua Kenya utapungua. Mkiwa nje ya federation, mbaki peke yenu, mtazungumza ukabila wenu. Hili ndilo nililoanza nalo. Nililoanza nalo niliposema Zanzibar sasa hivi wanasema sisi Wazanzibari. Sawasawa. Maana wamo ndani ya Muungano. Wamo ndani ya Muungano.

Kwa hiyo wanaweza kusema sisi Wazanzibari. Ninyi hapa mmo ndani ya Muungano. Kwa hiyo wendawazimu hapa wanasema sisi Watanganyika. Nje ya Muungano hamsemi hivyo. Nje ya Muungano mtasema sisi Wasukuma sisi Wanyamwezi sisi Wazaramo…

Advertisement