Hukumu kesi ya Maxence Melo yakwama kwa mara ya nne

Wednesday February 19 2020

 

By Fortune Francis, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Kesi ya kuzuia Jeshi la Polisi nchini Tanzania kufanya uchunguzi inayomkabili mkurugenzi mtendaji wa mtandao wa Jamii Forums, Maxence Melo na mwenzake Micke William imekwama kutolewa kwa mara ya nne.

Melo na William wanakabiliwa na kesi namba 456 ya mwaka 2016 ya kuzuia polisi kufanya uchunguzi.

Awali, kesi hiyo ilipangwa kutolewa hukumu Novemba 26, 2019 lakini iliahirishwa kutokana na Hakimu kutomaliza kuandaa hukumu na kupanga Desemba 29, 2019 lakini iliahirishwa kwa sababu hiyohiyo.

Ilipangwa kutolewa tena Januari 22, 2020 lakini iliahirishwa hadi leo Jumatano Februari 19, 2020 ambapo  hakimu anayesikiliza kesi hiyo, Thomas Simba hakuwepo mahakamani kwa kuwa ana majukumu mengine.

Wakili wa Serikali, Faraji Nguka amedai mbele ya Hakimu Mkazi mkuu, Huruma Shahidi kuwa kesi hiyo ilipangwa kwa ajili ya kutolewa hukumu lakini hakimu anayehusika hayupo.

Wakili wa utetezi,  Peter Kibatala amedai  wapo tayari kwa hukumu lakini kutokana na maelezo ya wakili wa Serikali hawana pingamizi.

Advertisement

Hakimu Shahidi ameahirisha kesi hiyo hadi Machi 19, 2020  kwa ajili ya kutajwa na Aprili 2, 2020 ndio itatolewa hukumu.

Katika kesi ya msingi, washtakiwa wanadaiwa kuzuia polisi  kufanya uchunguzi kinyume na Sheria namba 22 (2) cha Sheria ya Makosa ya Mtandano Namba 14 ya mwaka 2015.

Washtakiwa hao wanadaiwa kutenda kosa hilo kati ya Aprili Mosi, 2016 na Desemba 13, 2016  katika maeneo ya Mikocheni wilayani Kinondoni.

Advertisement