Idris aripoti tena polisi, makosa yake haya hapa

Muktasari:

Mchekeshaji na mshindi wa shindano la Big Brother 2014, Idris Sultan ameripoti kituo cha polisi kati leo Ijumaa Novemba Mosi, 2019 na kuhojiwa kwa dakika 30 na kutakiwa kuripoti tena Jumatano Novemba 6, 2019.

Dar es Salaam. Mchekeshaji na mshindi wa shindano la Big Brother 2014, Idris Sultan ameripoti kituo cha polisi kati leo Ijumaa Novemba Mosi, 2019 na kuhojiwa kwa dakika 30 na kutakiwa kuripoti tena Jumatano Novemba 6, 2019.

Jana asubuhi, Idris aliripoti kituoni hapo na kuhojiwa kwa saa tano na kupekuliwa nyumbani kwake,  usiku aliachiwa kwa dhamana akitakiwa kuripoti tena  leo saa 2 asubuhi, jambo ambalo amelitekeleza.

“Idris ameripoti kituoni saa 2:00 asubuhi na kuhojiwa kwa dakika 30. Wamechukua simu zake kwa uchunguzi na kutakiwa kuripoti tena Jumatano ijayo (Novemba 6, 2019).”

“Wamemueleza kuwa kosa lake ni kusambaza habari za uongo chini ya kifungu cha 16 cha sheria ya makosa ya mtandao. Kosa la pili ni kujifanya Rais chini ya kifungu cha 15 cha makosa ya mtandao,” amesema, Benedict Ishabakaki ambaye ni mwanasheria wa mchekeshaji huyo.

Jana alipopekuliwa nyumbani kwake polisi walichukua kompyuta mpakato kwa ajili ya uchunguzi, aliporudishwa kituoni kabla ya kupewa dhamana alipelekwa kitengo cha makosa ya mtandaoni.

Juzi mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda alimtaka Idris kuripoti polisi  baada ya kuweka picha yenye sura yake huku akiwa ameketi katika kiti chenye nembo ya Taifa.

Pia, Idris aliweka picha nyingine inayoonyesha sura ya Rais John Magufuli akiwa amesimama huku amevaa suruali yenye mikanda inayoshikizwa mabegani.

Hata hivyo, dakika chache baada ya Makonda kumtaka msanii huyo kuripoti polisi, waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamisi Kigwangalla aliahidi kumuwekea dhamana iwapo angekamatwa.

Ilivyokuwa

Mkasa ulianza kama masihara kwa Idris kuweka katika ukurasa wa mtandao wa kijamii wa Instagram picha yenye sura yake akiwa ameketi katika kiti chenye nembo ya Taifa huku akiandika “kwa siku moja tukabadilishana kazi ili a-enjoy siku yake ya kuzaliwa kwa amani.”

Baada ya kuweka picha hiyo, Makonda alichangia katika mtandao huo na kumtaka mchekeshaji huyo wa vituko vya ‘Sio Habari’ kujisalimisha polisi.

“Naona mipaka ya kazi yako huijui, nenda sasa hivi kituo chochote cha polisi uwaambie Makonda kaniambia nije utakuta ujumbe wako,” aliandika Makonda.

Baada ya mkuu huyo wa mkoa kueleza hayo, Dk Kigwangalla alishindwa kuvumilia badala yake akaandika katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Instagram, “nimeambiwa kuna msanii wa vichekesho anatafutwa na polisi. Mniambie nitajitolea mwanasheria wa kwenda kumuwekea dhamana na kumtetea. Rais wetu ni mtu wa watu na imejidhihirisha kwa jinsi wananchi walivyojitolea kumuombea dua siku ya kuzaliwa kwake. Wameonesha upendo.”

Alipozungumza na Mwananchi baadaye kuhusu sakata hilo, Makonda alisema “nimesema kweli aende polisi sina utani na watu wa aina hiyo.”

Kuhusu hatua ya Dk Kigwangalla kumwekea dhamana Idris iwapo atakamatwa, Makonda alisema “brother ile Twitt sikumuandikia mtu yeyote zaidi ya Idris, nenda kaisome vizuri.”