JANUARI 20 ILEE: Mshikemshike laini za simu

Tuesday January 14 2020
pic laini

Dar es Salaam. Hivi inawezekana laini za simu zaidi ya milioni 20 zikasajiliwa ndani ya siku saba?

Kama laini kama hizo zimeshindikana kusajiliwa kwa zaidi ya miezi tisa kuanzia Mei mwaka jana, itatumika miujiza gani kuhakikisha zinasajiliwa sasa?

Haya ni maswali unayoweza kujiuliza baada ya muda wa usajili wa laini hizo kwa alama za vidole kufikia mwisho Januari 20, mwaka huu.

Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa jana na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), zinaonyesha hadi kufikia Januari 7, mwaka huu laini zilizokuwa zimesajiliwa ni milioni 25 sawa na asilimia 52.42 ya laini milioni 48.

Takwimu hizo zilitolewa jana na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano kwa Umma kutoka TCRA, Frederick Ntobi alipozungumza na Mwananchi lililotaka kujua idadi ya laini zilizokuwa zimesajiliwa.

Usajili wa laini hizo umekumbwa na changamoto kubwa moja nayo ni wananchi kutokuwa na vitambulisho vya taifa au namba za utambulisho zinazotolewa na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida).

Advertisement

Katika maeneo mengi nchini kwenye ofisi za Nida kumekuwapo na foleni kubwa za wananchi wanaofika kujiandikisha ili wapate namba au vitambulisho lakini imekuwa ngumu kuvipata kwa wakati.

Kuzimwa kwa laini hizo kama ambavyo imeagizwa na Rais John Magufuli kunaweza kutikisa sekta ya fedha kwani kati ya asilimia 65 ya Watanzania wanaozitumia, asilimia 48 wanafanya hivyo kupitia simu za mkononi.

Taarifa ya TCRA kwa miezi sita iliyopita inaonyesha miamala ya zaidi ya Sh16 trilioni ilifanyika mpaka Juni mwaka jana.

Mamlaka hiyo inasema kwa robo ya kwanza iliyoishia Machi 30 mwaka jana, miamala ya Sh243.52 milioni ilifanyika ikiwa na thamani ya Sh7.82 trilioni huku miamala Sh260.43 milioni ikifanyika kati ya Aprili na Juni ikiwa na thamani ya Sh8.31 trilioni.

Katika hofu hiyo ya kuzimiwa laini zao, Desemba 31, Rais Magufuli alipunguza presha kwa wale ambao hawajajisajili kwa kuongeza siku 20 zaidi kuanzia Januari 1 hadi 20 zaidi ya hapo TCRA wazifunge laini.

Rais Magufuli alitoa maagizo hayo Desemba 27 mwaka jana mara baada ya kusajili laini yake kwa alama za vidole akiwa mapumzikoni nyumbani kwake Chato mkoani Geita.

Alisema usajili wa laini za simu kwa alama za vidole ni muhimu kwa usalama wa nchi ikiwamo kuepusha vitendo vya utapeli na ujambazi vinavyofanywa na wahalifu.

Mkazi wa Tabata jijini Dar es Salaam, Frank Ibrahim alisema ameshindwa kusajili laini yake kutokana na kutokuwa na kitambulisho. “Bado sijajua kama nitasajili au la kwani tatizo ni kitambulisho na ikitokea laini ikazimwa, sijui itakuwaje kwani simu hii ndiyo naitegemea kwa kila kitu.

“Hana natoa hela, nikitaka kutuma hela sijajua itakuwaje lakini ikikaribia muda wa kuzimwa, nitazitoa hela zangu zote zisije kuzimiwa humo,” alisema Ibrahim.

Mtazamo kiuchumi, njia mbadala

Mhadhiri Mwandamizi wa Uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Abel Kinyondo alisema kuna mambo mawili katika idadi hiyo ya laini mosi, wapo waliokuwa na laini zaidi ya tatu lakini usajili ulipoanza, wameamua kusajili zile wanazozihitaji tu na pili, wengine wameshindwa kutokana na kutokuwa na vitambulisho vya taifa.

Alisema kama watu wanashindwa kusajili kwa kutokuwa na vitambulisho, “hili litakuwa na athari kwani simu ni zaidi ya kila kitu, hata kama una simu ya kitochi bado utahitaji kuitumia kuwasiliana, kutoa fedha, kupokea au kutuma.”

Mwananchi lilipotaka kujua ni njia gani inaweza kutumika kwa walioshindwa kusajili kutokana na kutokuwa na vitambulisho, Dk Kinyondo alishauri kwa kuwa kuna vitambulisho vingi vinavyotolewa na mifumo ya Serikali yenye kuhitaji alama za vidole kama leseni, na cha kupigia kura vingeweza kutumika.

Alisema kwa muda uliobaki ni ngumu Nida kuweza kuwapatia wote wanaohitaji, “Serikali iangalie mifumo yake iweze kuwasiliana, kwani leseni au kitambulisho cha kupigia kura huwezi kukipata bila alama za vidole, mtu awe na uwezo wa kutumia kati ya hivyo kusajili laini yake kwani Tanzania siyo kisiwa.”

“Nida hata wakiongezwa miezi 12 hawawezi kuwamaliza wote kwani kila siku kuna watu wanafikisha miaka 18, kwa hiyo mimi nashauri Serikali iangalie njia ya kutumia mifumo yake iweze kuwasiliana na kupunguza usumbufu wanaokutana nao wananchi,” aliongeza Dk Kinyondo.

Rais Magufuli, Waziri Lugola

Suala hilo la vitambulisho au namba, limekwisha kuwaibua viongozi mbalimbali kulizungumzia na kutoa maagizo akiwamo Rais Magufuli kwa kumtaka Mkurugenzi Mkuu wa Nida, Dk Arnord Kihaule kuzunguka nchi nzima kushughulikia matatizo ya wananchi kukosa huduma hiyo.

Novemba 20 mwaka jana, Rais Magufuli alimtaka Dk Kihaule kufuatilia shughuli za utolewaji wa vitambulisho vya uraia nchi nzima.

Rais Magufuli alitoa maagizo hayo akiwa mkoani Morogoro baada ya wananchi wa Msamvu kumueleza adha wanazokumbana nazo wakati wa kujiandikisha kupata vitambulisho hivyo.

Kama hiyo haitoshi, Jumamosi iliyopita, Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola baada ya kupata malalamiko kutoka kwa wakazi wa Songea mkoani Ruvuma na Mtwara alikutana na Dk Kihaule mkoani Lindi na kumpa maagizo ya kuhakikisha anayafanyia kazi ili wananchi waweze kupata namba au vitambulisho.

Miongoni mwa maagizo hayo ni kuongeza wafanyakazi ili kuleta ufanisi, kuongeza muda wa kuhudumia wananchi waliofika eneo la kazi na wasiondoke kazini hadi waishe ikiwamo kufanya kazi siku za mapumziko za mwisho wa wiki.

Lugola pia aliwataka watumishi wa Nida kuwatumia wananchi namba zao kupitia simu zao za mkononi.

Advertisement