Kakunda, Hasunga wataka viwanda vya kuchakata mazao Kyela

Muktasari:

Waziri wa Viwanda na Biashara, Joseph Kakunda amesema ingawa Kyela inazalisha mazao mengi na kuwa na masoko ya kimataifa, ni vyema kukaanzishwa viwanda vikubwa kwa ajili ya kuchakata mazao yanayozalishwa ili kukuza uchumi

Dar es Salaam. Waziri wa Viwanda na Biashara, Joseph Kakunda amesema ingawa Kyela inazalisha mazao mengi, kuwa na masoko ya kimataifa ni vyema ikaanzisha viwanda vikubwa kwa ajili ya kuchakata mazaoili kukuza kiuchumi.

Kakunda amesema wizara yake kwa kushirikiana na mbunge wa Kyela wanafanya utaratibu wa kuhakikisha viwanda vinajengwa ili mazao mengi yanayozalishwa yaweze kuongezwa thamani  hapohapo kwa kuwa mazingira ya biashara ni makubwa katika eneo hilo.

Kakunda ametoa kauli hiyo leo Aprili 30 katika viwanja vya Mwakangale wilayani Kyela katika ziara ya Rais John Magufuli mkoani Mbeya.

“Mazingira ya viwanda na biashara ni makubwa hapa Kyela, wanazalisha mpunga kilo milioni 68 kwa nini msiwe na kiwanda kikubwa cha kuchakata mpunga na kupaki mchele kwa ajili ya  soko la kimataifa?”

“Tutawasaidia kuwaletea viwanda, cocoa inazalishwa tani 8,250 ina maana mnahitaji kiwanda cha kuchakata  cocoa hapa mtengeneze chocolate lazima twende na mazingira yanayohitajika kibiashara, nitamwagiza meneja wa Sido mkoa aweke kambi Kyela ili kusaidia viwanda vidogovidogo,” amesema Kakunda.

Awali Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga amesema mazao yanazalishwa kwa wingi eneo hilo na kwamba Kyela ni eneo linalozalisha chakula kwa wingi.

“Wapo watu walikuwa wanatumia eneo hili kwa maslahi binafsi na aliyekuwa analeta shida tulishamuondoa tutahakikisha pembejeo zinapatikana na wakulima wanaendelea kulima,” amesema Hasunga.