Kalemani akagua mradi wa umeme utakaowanufaisha wananchi 10,000

Muktasari:

  • Waziri wa Nishati nchini Tanzania, Dk Medard Kalemani amekagua mradi wa ujenzi wa kusafirisha umeme wa Kenya-Tanzania Power Interconnection Project (KTPIP) ambao utawanufaisha watu 10,000 katika vijiji 19 vilivyopo katika ya Singida na Namanga.

Dar es Salaam. Waziri wa Nishati nchini Tanzania, Dk Medard Kalemani amekagua mradi wa ujenzi wa kusafirisha umeme wa Kenya-Tanzania Power Interconnection Project (KTPIP) ambao utawanufaisha watu 10,000 katika vijiji 19 vilivyopo katika ya Singida na Namanga.

Kalemani amekagua mradi huo  eneo la Lemuguru wilayani Arumeru Mkoa wa Arusha kilipo kituo cha kupoza umeme wa mradi mzima wenye urefu wa kilometa 414.

Kalemani amesema mbali na wanufaika pia Tanzania itaunganishwa katika Gridi ya Taifa na mataifa washirika ya ukanda wa Afrika Mashariki kupitia muungano wa mfumo wa usafirishaji umeme wa pamoja wa East African Power pool (EAPP) ukijumuisha nchi washirika takribani 11.

“Nimekuja kukagua na kujionea maendeleo ya ujenzi wa mradi ulioanzia Singida mpaka Namanga ukiambatana na uunganishaji umeme wa wateja 10,000 katika vijiji 19 vilivyopo kandokando ya laini kuanzia Singida mpaka hapa,” amesema Kalemani.

Kalemani amebainisha kuwa kukamilika kwa mradi huo kutaifanya Tanzania kuwa nchi ya kwanza yenye miundombinu tayari kwa kuanza biashara ya kuuza, kununua ama kusafirisha umeme katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Kalemani amemtaka mkandarasi wa mradi huo na Shirika la Umeme (Tanesco) kuongeza kasi ya ujenzi ili kumaliza mapema, kwamba hadi sasa umefikia asilimia 40, “mradi mzima umefikia asilimia 61.2.”