Kampeni elimu kwa mlipakodi kuanza Dar

Muktasari:

 Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imeanzisha kampeni ya huduma na elimu kwa mlipakodi katika Mkoa wa Dar es Salaam itakayofanyika kwa siku tatu kuanzia kesho Desemba 2 hadi 14, 2019.

Dar es Salaam. Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imeanzisha kampeni ya huduma na elimu kwa mlipakodi katika Mkoa wa Dar es Salaam itakayofanyika kwa siku tatu kuanzia kesho Desemba 2 hadi 14, 2019.

Akizungumzia kampeni hiyo jana jijini Dar es Salaam, mkurugenzi wa Idara ya Huduma na Elimu kwa Mlipakodi wa TRA, Richard Kayombo amesema lengo ni kutoa elimu kuhusu masuala mbalimbali ya kodi pamoja na kusikiliza malalamiko, changamoto na kupokea maoni kutoka kwa wafanyabiashara na wananchi.

"Kampeni hii ni mwendelezo wa kampeni ambayo imemalizika katika Mikoa ya Morogoro na Pwani na sasa tunaingia katika Mkoa wa Dar es Salaam tukiwa na lengo la kuwaelimisha walipakodi na wananchi masuala yanayohusu kodi, kupokea maoni yao, kusikiliza changamoto na malalamiko ili tuweze kuyatafutia ufumbuzi,” amesema Kayombo.

Kayombo amesema kampeni hiyo itaambatana na huduma ya usajili wa wafanyabiashara wapya wasiokuwa na namba ya utambulisho wa mlipakodi.

"Pamoja na kutoa elimu ya kodi, kupokea maoni na kusikiliza changamoto za walipakodi pia tutatoa huduma ya usajili wa walipakodi wapya ambapo tutawapatia cheti cha namba ya utambulisho wa mlipakodi tukiwa na dhumuni la kupanua wigo wa walipakodi  nchini,” amesema.

Kayombo amebainisha maeneo yatakayofikiwa katika kampeni hiyo kuwa ni Ilala, Kinondoni, Temeke na Kariakoo na itakuwa semina katika vituo vilivyopangwa kwenye maeneo hayo pamoja na kuwatembelea walipakodi katika biashara zao yaani duka kwa duka.