Kauli tatu tata za Waziri Jafo uchaguzi wa serikali za mitaa

Muktasari:

  • Tanzania itafanya uchaguzi wa serikali za mitaa Novemba 24, 2019 ambapo tangu mchakato wake ulipoanza, Waziri wa Tamisemi, Seleman Jafo amekuwa akitoa kauli mbalimbali zinazoibua mijadala kwa wadau.

Dar es Salaam. Uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika Novemba 24, 2019 zimembainisha Waziri wa Tamisemi, Seleman Jafo katika sura tatu tofauti.

Uchaguzi huo umekuwa na sintofahamu baada ya vyama vitano vya upinzani kutangaza kwa nyakati tofauti kutoshiriki kwa madai ya wagombea wao kutokutendewa haki ikiwamo kutopewa fursa ya kurejesha fomu au kuzichukua.

Vyama hivyo ni Chadema, UPDP, ACT- Wazalendo, Chaumma pamoja na NCCR-Mageuzi.

Kauli ya kwanza ya Jafo ni ile aliyoitoa Novemba 7, 2019 muda mfupi baada ya Chadema kutangaza kutokushiriki uchaguzi huo.

Waziri Jafo alisema uamuzi huo unawanyima fursa wagombea wa chama hicho waliopitishwa, waliokata rufaa kupinga kuenguliwa.

Katika maelezo wakati wa mkutano na waandishi wa habari Mjini Dodoma Jafo alisema ingawa ni haki yao lakini ameshangazwa na uamuzi wao kwa sababu kila kitu kipo wazi. Kanuni haijafunga mtu yeyote kukata rufaa.

Uamuzi wa Chadema ulitangazwa na Mwenyekiti wake, Freeman Mbowe mjini Dodoma baada ya kumalizika kikao cha dharura cha kamati kuu ambapo katika maelezo yake alisema kuendelea kushiriki uchaguzi huo ni kuhalalisha ubatili akibainisha takribani asilimia 85 ya wagombea wao nchi nzima wameenguliwa.

Novemba 9, 2019, Waziri Jafo alitoa kauli ya pili katika harakati za uchaguzi huo baada ya kusema vyama ndio vimejitoa katika uchaguzi huo na sio wagombea.

“Katika uchaguzi wa mwaka 2019, wagombea waliojitokeza na kuchukua fomu ni 550, 036 na ambao walirejesha fomu kwa wakati ni 539,953 sawa na asilimia 97.29,”

“Kwa hiyo ambao hawakurejesha fomu labda kwa sababu mbalimbali au kwa matakwa yao binafsi ni 10, 083 sawa na asilimia 2.1 tu,” alisema Waziri Jafo wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari mjini Dodoma.

Kauli ya tatu ya Waziri Jafo aliitoa jana Jumapili Novemba 10, 2019, katika mkutano wake na waandishi wa habari mjini Dodoma Jafo alitangaza kuwarejesha wagombea wote wa Serikali za mitaa  ambao walichukua fomu na kuzirejesha.

Alisema uamuzi huo hautawahusu wagombea ambao si raia wa Tanzania na wale ambao hawajajiandikisha katika kijiji, mtaa ama kitongoji husika.

Wengine ambao hawahusiki ni waliojiandikisha kupiga kura mara mbili, waliojidhamini wenyewe, hajadhaminiwa na chama chake cha siasa, wamerejesha fomu watu zaidi ya mmoja kutoka chama kimoja kwa nafasi inayofanana ya uenyekiti wa kijiji au kitongoji, mtaa au kitongoji husika.