Kesi ya DC Chemba: Ulimuoa mkiwa vijana, leo uzeeni unataka kumuacha ili aolewe na nani

Muktasari:

Kesi ya madai ya talaka namba 181 /2019 iliyofunguliwa na Mkuu wa Wilaya ya Chemba (DC), jijini Dodoma nchini Tanzania, Simon Odunga imeendelea kwa hatua ya ushahidi ambapo shahidi katika kesi hiyo ameiomba Mahakama ya Mwanzo Ukonga Dar es Salaam isikubali kuivunja ndoa kati ya Ondunga na Medilina Mbuwuli iliyofungwa kanisani mwaka 2000

Dar es Salaam. Ruth Osoro  ambaye alikuwa anajitambulisha kuwa mke wa mkuu wa wilaya ya Chemba (DC), jijini Dodoma, Simon Odunga ametinga katika Mahakama ya Mwanzo ya Ukonga, Dar es Salaam kutoa ushahidi dhidi ya ndoa iliyofungwa kanisani baina ya ‘mumewe’ huyo na Medilina Mbuwuli mwaka 2000.

Osoro aliyekuwa amefunga ndoa bomani na Odunga kabla ya Mahakama kusema haiitambui ndoa hiyo kwa madai mkuu huyo wa wilaya alikwisha kufunga ndoa ya kanisani hivyo ndoa zingine zinazofuata ni batili.

Ushahidi huo ameutoa leo Jumanne Septemba 3,2019 mbele ya Hakimu Christina Luguru katika kesi ya madai ya talaka namba 181 /2019 iliyofunguliwa na Odunga dhidi ya Mbuwuli.

Hata hivyo, Septemba 13, 2019 hukumu ya kesi hii itatolewa na Hakimu Luguru baada ya kusikiliza ushahidi wa mashahidi wa pande zote mbili na kufunga ushahidi wao.

Akitoa ushahidi kwenye kesi hiyo, Osoro ameiomba mahakama isivunje ndoa ya mke mwenzie huyo kwa sababu mdai Odunga hana sababu za msingi za kuvunja ndoa hiyo bali anashinikizwa na hawala.

Pia,  ameiomba Mahakama isiivunje ndoa hiyo kwa sababu ni ndoa takatifu ya kanisani iliyofungwa baina ya Medilina na Odunga na kwamba wawili hao waliapa kuishi katika shida, ugonjwa na raha hadi hapo mauti yatakapowatenganisha.

Akitoa ushahidi katika kesi hiyo, Osoro ameiambia mahakama yeye na Odunga walifunga ndoa mwaka 2010 na kwamba wakati wakifunga ndoa Odunga hakuwahi kumueleza ana ndoa ya kanisani bali alimueleza alikuwa na mwanamke lakini walikuwa hajafunga ndoa.

“Laiti kama ningekuwa najua kwamba alikuwa ana ndoa ya kanisani nisingekubali kufunga ndoa  hiyo. Alieleza Osoro mahakamani hapo,” amesema

“Baada ya kunioa tuliendelea kuishi  lakini nilibaini kuwa Odunga alikuwa na ndoa ya kanisani mwaka 2013 kupitia ndugu zake na kwamba kipindi hicho alikuwa akipotea wiki moja, mbili ama tatu kumbe alikuwa akifanya siri,” amesema

Akiendelea kutoa ushahidi amesema, katika ndoa hizo yeye alipata mtoto mmoja wa kiume ambaye kwa sasa ana umri wa miaka 4 na Medilina ana mtoto wa kike mwenye umri wa miaka 18 anasoma kidato cha sita.

Amesema baada ya kubaini Odunga alikuwa na ndoa takatifu ya kanisani, alimtafuta Mbuwuli wakazungumza wakaelewana na hadi sasa wanaishi kwa kupendana na kuheshimiana.

Amesema Odunga amedanganya kwa kuwa aliona cheti cha ndoa ya Kikristu aliyofunga mwaka 2000 na Medilina aliapa ndoa ya mke mmoja na katika cheti changu cha ndoa tuliyofunga mwaka 2010 bomani napo pia aliapa ndoa ya mke mmoja na kwamba hajawahi kuoa kumbe si kweli.

“Mheshimiwa hakimu, nakuomba hii ndoa isivunjwe hadi umauti utakapowatenganisha kwa sababu mdai Odunga hana sababu za msingi za kutaka kutoa talaka,” amesema Osoro.

Amesema yeye aliwahi kuambiwa na Odunga alikuwa na mwanamke lakini hawakuwahi kufunga ndoa ndiyo maana alikubali kufunga naye ndoa na kwamba iwapo angefahamu kuwa mkuu huyo wa wilaya amekwisha funga ndoa takatifu ya kanisani asingekubali.

Osoro amedai yeye alibaini Odunga alikuwa ana ndoa ya kanisani mwaka 2013 baada ya kuwa amekwisha olewa naye na alifahamu kupitia ndugu zake wa karibu na kipindi hicho walipokuwa wakiishi Odunga alikuwa akiondoka wiki moja ama mbili hayupo nyumbani kwake kumbe alikuwa akienda kwa mke wake Medilina ama Latifa (alimtaja kwa jina moja).

“Mimi nilikuwa mke wa Odunga kwa kunidanganya,  mimi ulinidanganya kuwa hujawahi kuoa, tukafunga ndoa bomani, siyo mimi tu uliyenidanganya hata serikali pia uliidanganya,” amesema Osoro na kuongeza “ulimuoa mkiwa vijana leo uzeeni unataka kumuacha ili aolewe na nani.”